TUCTA yataka Serikali kuharakisha fao la kujitoa - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

.

.

Tuesday, May 2, 2017

TUCTA yataka Serikali kuharakisha fao la kujitoa

Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ili wafanyakazi wapate haki yao.

Limeitaka pia kuangalia upya makato ya kodi ya mishahara ili yanufaishe watumishi wote na kueleza kuwa kilichopunguzwa mwaka jana kinalinda wafanyakazi wachache wa kima cha chini cha mishahara.

Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa, alisema hayo kwenye hotuba ya Shirikisho hilo mbele ya Rais John Magufuli kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mjini Moshi, Kilimanjaro jana.

Alisema kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa wakisubiri upitishwaji wa fao hilo ambalo litawasaidia kujikimu wanapokosa ajira huku akiongeza kuwa kiwango cha kodi ya asilimia tisa kinachotozwa kinanufaisha watumishi wa mshahara wa kima cha chini.

“Tunaiomba Serikali iharakishe kuanzisha fao la kukosa ajira, ili linufaishe wafanyakazi. Kingine vikokoteo vya mafao ya mifuko ya jamii viboreshwe ili watumishi waone matunda ya kuchangia,” alisema Dk Msigwa.

Aliishauri Serikali kufanya maboresho kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo kuunda mifuko miwili wa umma na wa binafsi ili kuondoa mkanganyiko wa vikokoteo uliopo, wingi wa mifuko ya hifadhi na kupunguza muda wa wastaafu kusotea mafao.

Alifafanua, kwamba baada ya Serikali kupunguza kiwango cha kodi ya mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi tisa, TUCTA imebaini wafanyakazi wanaopokea mishahara ya kima cha chini ndio wanufaika wakubwa, huku wenye kima cha juu wakiendelea kubanwa.

Kuhusu wawekezaji, Dk Msigwa alisema wapo wanaokiuka sheria za kazi na kanuni za ajira, ikiwamo kunyima wafanyakazi haki ya kuunda vyama vya kutetea maslahi yao, pamoja ulipaji mishahara kibaguzi.

Alibainisha kuwa wapo wawekezaji wanaolipa watumishi wenye Shahada kutoka nje ya nchi Sh milioni saba na kuwalipa wazawa Sh 700,000.

Aidha, aliiomba Serikali kuzifanyia maboresho sheria za utumishi wa umma zinazohusu uhusiano wa kazi ili ziwawezeshe kupeleka masuala yao kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Kazi (CMA).

Pia aliitaka Serikali kuwezesha majaji kwenda mikoani kumaliza usikilizaji kesi za wafanyakazi kwa wakati na haki itendeke huku akibainisha kuipunguzia majukumu Wizara ya Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ili ishughulikie matatizo ya wafanyakazi.

Alisema TUCTA inaipongeza Serikali kwa kupambana na rushwa, ufisadi, kuondoa watumishi hewa, kupambana na dawa za kulevya na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi
Post a Comment