ICS YAZINDUA MRADI WA MAJI WILAYANI KISHAPU, SHINYANGA. - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

.

.

Wednesday, July 12, 2017

ICS YAZINDUA MRADI WA MAJI WILAYANI KISHAPU, SHINYANGA.

Wananchi Zaidi ya 15,000 wa vijiji vya Maganzo na Masalaga sasa wananufaika na maji safi baada ya shirika la ICS kukamilisha na kuzindua rasmi mradi huo. Uzinduzi wa mradi wa maji safi umefanywa na kiongozi wa mbio za mwenge Bwana Amour Ahmad Amour kwa niaba ya serikali.  Uzinduzi huo umewapa fursa wananchi hao kuanza kutumia maji kwa mfumo wa malipo ya kabla ambapo maji yanapatikana kwa masaa 24 kila mwananchi akichota kwa muda wake kwa kutumia kadi maalum kulingana kiasi anachokihitaji.
 Shangwe za uzinduzi wa mradi wa maji zilisindikizwa na hotuba fupi kutoka kwa mkuu wa msafara wa mbio za mwenge akiwataka wananchi kuitumia neema hiyo kwa uangalizi mkubwa kwani teknolojia yake ni ya kisasa na adimu  sana akiwapa mfano kuwa katika Tanzania nzima teknolojia hii ipo Dodoma tu ya ununuaji maji kwa mfumo wa malipo ya kabla. Hivyo uharibifu wa miundo mbinu utawagharimu wananchi wenyewe kuikosa huduma hiyo. Pia aliwataka ICS kuendelea kutoa huduma za kijamii hasa zinazomwangilia mama na mtoto wa kike katika kuhakikisha wanapata maji kiurahisi ili nao waweze kufanya shughuli za uzalishaji pamoja na watoto kuzingatia masomo.
 Akiongea kwa niaba ya Shirika la ICS, Mkurugenzi wa Shirika hilo Bwana Jonathan Kifunda amewataka wananchi wa Kishapu kuyatumia maji hayo kwa uhuru kabisa kwani sasa mradi huo umezinduliwa rasmi. “Tumetumia milioni mia saba hamsini na tano kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa ajili ya wananchi wa Maganzo na Masagala kupata maji kiurahisi.  “Kufuatia wananchi kufuata maji umbali mrefu na kuyanunua kwa gharama kubwa kwa miaka yote iliyopita. ICS tuliona ipo haja ya kuwasaidia wananchi hawa kwa kuwapatia maji safi ya ziwa Victoria. Sasa tumezindua vituo 25 ndani ya vijiji viwili, tumeweka vocha za kununulia Maji katika maduka ya hapa hapa vijini kwao kwa hiyo mwananchi utatakiwa kuweka vocha katika tokeni yako na kununua kiasi ukitakacho cha maji”.
 Mkuu wa wilaya ya Kishapu Bi Nyabaganga Talaba ameipongeza ICS kwa kupigania jamii ya mkoa wa Shinyanga hasa kwa kutotoa msaada bali kuwawezesha wananchi. Pia amewataka wananchi hao kuwa walinzi wa mradi na kuyatumia maji vyema huku akiwapa neno la muhimu kuwa “Haya ni maji safi, tuyatunze yadumu”.
Post a Comment