RC Paul Makonda Atimiza Ahadi yake ya Misaada ya Milioni 164 - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, December 15, 2016

RC Paul Makonda Atimiza Ahadi yake ya Misaada ya Milioni 164

Mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekabidhi vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 164 alivyoahidi kwenye ziara zake na pikipiki tano kwa Saidi Mrisho aliyetobolewa macho na ‘Scorpion’.

Kuanzia Novemba 19 hadi 28, Makonda alifanya ziara katika wilaya za Dar es Salaam kujua matatizo ya wananchi na kuahidi kutekeleza baadhi ya mambo.

Akizungumza jana, Makonda alisema ameona ni vema akaanza kutekeleza baadhi ya ahadi zake kabla mwaka kumalizika, huku mambo mengine yakisubiri utekelezaji kutoka ngazi za juu za uongozi.

Makonda alikikabidhi kituo cha kurekebisha tabia cha Kigamboni magodoro 50, runinga, king’amuzi, mitungi miwili ya gesi na jiko.

Pia alikabidhi gari la kubeba wagonjwa kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Ukonga, na tumba za kwaya ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Sekondari ya Jitegemee ilipewa mabati 2,000, shule ya msingi Mbagala Annex mabati 1,000, shule ya Katoliki mifuko 10,000 ya saruji, soko la samaki Msasani mabati 300, kanisa la AIC matofali 10,000 na mabati 200 kwa ajili ya Uwanja wa Taifa.

Katika kuthamini viongozi wanaojituma, alitoa pikipiki kwa mtendaji wa kata ya Mbuyuni na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buguruni.

Pia hakuwaacha nyuma wajasiriamali kwani alimkadidhi Lumino Evance mtaji wa Sh milioni moja na mama muuza machungwa Zuhura Waziri mtaji wa Sh 200,000.

Kutokana na changamoto ya maji Ukonga, Makonda alikabidhi Sh milioni 13 ili wananchi wa Gongo la Mboto na Pugu wapate maji. Pia alitoa Sh 500,000 kwa ajili ya kukamilisha tangi la maji kwa wananchi wa Buyuni, kata ya Pemba Mnazi.

Aidha, Makonda alitoa zawadi kwa watumishi wanne waliokuwa  tayari kujitolea na kufanya kazi kwa ufanisi, ambao walizadiwa kulala  siku moja kwenye hoteli ya kifahari kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni tano.

Kuhusu Mrisho ambaye alishindwa kuhudhuria hafla hiyo na kuwakilishwa, Makonda alisema utaratibu wa kumtafutia nyumba kama alivyoomba unaendelea.

Aliongeza kuwa kilichokwamisha ni eneo alilochagua ambalo walikuta lina mgogoro, hivyo alisema wanamtafutia sehemu nyingine kwa sasa.

Baada ya makabidhiano hayo baadhi ya wanufaika walimshukuru Makonda kuwa mwenye moyo wa uthubutu.

Kamanada wa FFU Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Stanley Kukaganeo alisema gari walilokabidhiwa litasaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi wanaohitaji msaada wa dharura.

“Tumekuwa tukiumia sana mgonjwa kufia mikononi mwetu kwa sababu ya kukosa gari la kumwahisha hospitali ila Mkuu wa Mkoa tulikueleza hilo na sasa umetekeleza, ahsante sana,” alisema.

Zuhura alisema hakuwahi kufikiria kitu kama hicho katika maisha yake na anaona ni bahati kupata msaada huo.

“Niliomba Sh 20,000 ila wewe (Makonda) umenipa Sh 200,000, Mungu akubariki na uendelee na moyo huo huo wa kutusaidia,” alisema.
Kamanda wa kikosi cha kutuliza ghasia kanda maalum ya Dar es Salaam, Acp.Stanley Kulyamo akipokea gari la wagonjwa kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda jana Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam , Paul Makonda akikabidhi zawadi  tumba kwa ajili ya bendi ya jeshi la Wananchi mara baada ya kufanya vizuri katika mahadhimisho ya miaka 55 ya uhuru.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda , akikabidhi  shilingi laki mbili kwa mjasiliamali ,Zuhura Waziri mkazi wa Mwembe Yanga kwa ajili ya kuongeza mtaji wake wa Supu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda akikabidhi mifuko ya Saruji kwa Mkuu wa shule ya St Joseph Goba , Sister Caroline Kokutekana, kama sehemu ya kutimiza ahadi yake wakati wa mahafali ya shule hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda akikabidhi mabati  kwa mkuu wa shule ya sekondari  Jitegemee kama sehemu ya ahadi yake katika kampeni ya Dar es Salaam mpya.
Loading...

No comments: