Watu 10 Watiwa Mbaroni Kwa Kumchapa Mwanamke Viboko 30 Rorya - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, January 11, 2017

Watu 10 Watiwa Mbaroni Kwa Kumchapa Mwanamke Viboko 30 Rorya

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya mkoani Mara, linawashikilia watu 10 kwa udhalilishaji wa kumchapa viboko mwanamke hadharani.

Watu hao ni wa kijiji cha Kinesi tarafa ya Suba wilayani Rorya. Miongoni mwa watu hao, wamo viongozi watano wa baraza la mila liitwalo Irienyi ndogo la kabila la Wasimbiti.

Watu hao wanatuhumiwa kumchapa viboko zaidi ya 30 hadharani mwanamke huyo, kitendo kilichomdhalilisha mbele ya jamii.

Mapema wiki hii, baadhi ya video ilisambaa katika mitandao ya kijamii, ikimuonesha mwanamke akichapwa viboko na wanaume kwa zamu huku akilia mbele ya hadhara na sauti za wanaume zilisikika zikishabikia kitendo hicho.

Kamanda wa Polisi Tarime/ Rorya, Andrew Satta alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 23 mwaka jana mchana katika kitongoji cha Migutu kijiji cha Kinesi tarafa hiyo ya Suba wilayani Rorya katika maeneo ya Mastooni, ambako kulikuwa na mkutano wa Ritongo wa mila.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa kijiji hicho (jina limehifadhiwa) aliitwa na kufuatwa na vijana na kupelekwa katika mkutano huo wa mila, uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa kijiji hicho. Ilidaiwa kuwa mwanamke huyo alimtuhumu mama yake mzazi wa umri wa miaka 55 kuwa ni mchawi.

Kwamba hamtambui na kumkana kuwa si mama yake mzazi; huku akidai kuwa mama huyo anataka kumuua kwa uchawi. 

Kamanda Satta alisema katika mkutano huo wa baraza la mila la Irienyi, vijana sita waliamriwa kumchapa kila mmoja viboko vitano makalioni mwanamke huyo, hali iliyomsababishia majeraha, kumuathiri, kumdhalilisha na kumshushia utu wake kwa jamii.

“Tumewakamata mwenyekiti wa baraza hilo, viongozi wenzake wanne na vijana sita walioshiriki kumkamata na kuadhibu kwa kumlaza chini, kumchapa viboko na kumsababishia madhara makubwa mwilini na kumdhalilisha,” alisema Kamanda. Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na jeshi hilo linaendelea kuwasaka wengine waliohusika.
****


==>Video ya tukio
 
A
Loading...

No comments: