Waziri Mkuu Akemea Uharibifu Wa Mazingira - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, January 2, 2017

Waziri Mkuu Akemea Uharibifu Wa Mazingira

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya wakazi wa Ruangwa wanaokata miti kwenye misitu waache kufanya hivyo mara moja ili kuokoa ardhi chepechepe waliyokuwa nayo.

Amesema ukataji miti huo unafanywa zaidi na watu wanaoanzisha mashamba ya ufuta na wapo walioamua kulima karibu na vyanzo vya maji hali iliyosababisha maji yakauke kwenye maeneo mengi.

“Zamani kuna maeneo ulikuwa haupiti hadi ukunje suruali, na kama una gari napo pia ilikuwa ni taabu kupita kwenye maeneo hayo. Lakini sasa hivi, hakuna tena maeneo hayo ndiyo maana kila unakopita unakuta akinamama wanatembea mwendo mrefu na ndoo huku vijana wakibeba madumu kwenye baiskeli nao wakitafuta maji,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa.

Ametoa onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa vijiji mbalimbali vya  wilaya hiyo ambao walifika Ruangwa mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM kusikiliza taarifa ya mambo aliyoyafanya jimboni humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

“Kilimo cha ufuta kimekuwa balaa, sasa hivi hakuna maji sababu ya ukataji miti ovyo. Mfano mzuri ni mto Mbwemkuru ambao ulikuwa ukitiririsha maji mwaka mzima, angalia sasa hivi, umegeuka kuwa mto wa msimu na chanzo ni ukataji wa miti,” alisisitiza.

“Tusipobadilika na kuacha hiyo tabia tutamlaumu mbunge na Serikali kuwa hawaleti maji wakati sisi wenyewe tumechangia hali hiyo kwa kuharibu vyanzo vya maji,” alionya na kuongeza kuwa amelazimika kutafuta mashine ya kuchimba maji ili kupunguza tatizo la maji.

Alisema mapema mwaka huu, wataalamu wataanza kufanya utafiti ili kubaini maji yako umbali gani kwenda ardhini kabla ya kuanza kuchimba visima hivyo. “Ikibidi tutaaza na visima vifupi na vya kati ili maji yapatikane haraka,” alisema.

Akielezea mipango ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi wa jimbo hilo kwamba anatamani kuona kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa vijijini.

“Kila nilikopita vijijini nimewahamasisha wananchi waanze kufyatua mafotali ili ujenzi wa boma ya zahanati uanze. Na mimi nimeahidi kuchangia mabati kwa kila zahanati, na kuna baadhi ya maeneo nimechangia hata mabati ya nyumba ya mganga na muuguzi,” alisema.

Alisema mwaka uliopita, alifanikiwa kukamilisha ujenzi wa wodi ya akinababa, ya akinamama na kukarabati wodi ya magonjwa mchanganyiko katika hospitali ya wilaya ambapo fedha taslimu milioni 100 zilitumika. Pia aliwezesha kufunga umeme wa jua kwenye zahanati zote zinazotoa huduma za afya ndani ya jimbo na kazi hiyo itaendelea kwa awamu ya pili.

“Pia niliweza kulipia kaya 10 zisizokuwa na uwezo kwa kila kijiji ili zijiunge na mfuko wa afya ya Jamii (CHF) kwa gharama za shilingi milioni 9. Jumla ya vijiji 92 vimefikiwa. Ninawasihi wana-Ruangwa kila mmoja ajiunge na mfuko huu ili muweze kupatiwa huduma za afya bila matatizo,” aliongeza.

Akielezea kuhusu sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema ameweza kufadhili ujenzi wa matundu ya vyoo 70 Katika shule za msingi saba ambapo kila shule imejengewa matundu 10 (manne wavulana, manne wasichana na mawili kwa walimu) ambapo jumla ya sh. milioni 63 zimetumika. Alisema kazi hiyo itaendelea awamu ya pili.

“Zaidi ya hayo, nimefanikisha ufungaji wa umeme jua kwenye shule za sekondari nne za Chunyu, Makanjiro, Narungombe na Nambilanje. Katika awamu ya kwanza tumekamilisha kuweka umemejua kwenye sekondari za tarafa ya Mandawa, na tarafa ya Ruangwa imefikiwa nusu tu. Katika awamu ya pili, tutamalizia tarafa ya Ruangwa na kukamilisha tarafa nzima ya Mnacho,” alisema.


IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, JANUARI 2, 2017.
Loading...

No comments: