Wafanyakazi wengine Wawili wa Quality Group ya Yusuf Manji Wafikishwa kizimbani - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, February 28, 2017

Wafanyakazi wengine Wawili wa Quality Group ya Yusuf Manji Wafikishwa kizimbani

Wafanyakazi wengine wawili wa Kampuni ya Quality Group inayomilikiwa na Yusuf Manji ambao ni raia wa India wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuzuia maofisa wa Uhamiaji kutimiza majukumu yao.

Washitakiwa hao ni Jose Kiran (40) ambaye ni Meneja Miradi wa kampuni na Prakash Bhatt (35) ambaye ni Katibu Muhtasi wa kampuni hiyo ambao wameongezwa katika kesi inayowakabili wafanyakazi 14 wa kampuni hiyo, raia wa India wanaokabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la kughushi viza ya biashara.

Wakili wa Serikali, Method Kagoma alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu Namba 30 (1) (f) na Kifungu Namba 2 cha Sheria ya Uhamiaji ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Namba 8 ya Mwaka 2015.

Kagoma alidai washitakiwa hao wawili, Februari 20 mwaka huu katika Kampuni ya Quality Group waliwazuia maofisa Uhamiaji kutimiza majukumu yao baada ya kukataa kuripoti kwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kujaribu kukimbia nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro.

Washitakiwa wote walikana mashitaka ambapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo upande wa mashitaka unaomba tarehe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Hata hivyo, washitakiwa waliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano.

Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo itatajwa Machi 7 mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali. 

Mbali na washitakiwa hao, wengine katika kesi hiyo ni Rajat Sarkar (35), Jagadish Mamidu (29), Niladri Maiti (41) Divakar Raja (37) ambao ni washauri wa kampuni hiyo, huku Mohammad Shaikh (44) mhasibu na Pintu Kumar (28) ambaye ni Meneja msaidizi wa kampuni.

Pia wapo ni Bijenda Kumar (43), Prasson Mallik (46), Nipun Bhatt (32), Anuj Agarwal (46), Varun Boloor, Arun Kateel (46), Avinash Chandratiwari (33) na Vikram Sankhala (50) ambao wote ni washauri wa kampuni hiyo. Kagoma alidai katika mashitaka ya kwanza washitakiwa walitenda kosa hilo Februari 13, mwaka huu maeneo ya Kampuni ya Quality Group, Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Alidai kuwa washitakiwa wote wakiwa ni raia wa nchini India, walikutwa na visa zilizoghushiwa kinyume na kifungu namba 31 (1) (e) na Kifungu Namba 2 cha Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 8 ya mwaka 2015. Kagoma alidai katika mashitaka ya pili kuwa washitakiwa wote kwa pamoja katika tarehe hiyo hiyo, mwaka huu, maeneo ya Kampuni ya Quality Group, walikutwa wakiishi nchini kinyume na sheria.

Pia katika mashitaka ya tatu, inadaiwa washitakiwa wakiwa katika Kampuni hiyo, huku wakijua kuwa wao ni raia wa India walikutwa wakifanya kazi nchini kinyume na kifungu namba 9 (i) (e) na kifungu namba 3 cha sheria ya ajira namba 1 ya mwaka 2015.

Hivi karibuni, Ofisi ya Uhamiaji ilitaja wafanyakazi 25 wa Yusuf Manji kwamba wanafanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali na kukusudia kumfungulia mashitaka mfanyabiashara huyo ambaye pia anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya, kwa kosa la kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi wasio na vibali.
Loading...

No comments: