Waziri Mkuu: Tutahakikisha Wauza Madawa ya Kulevya Wote Wanakamatwa - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, April 25, 2017

Waziri Mkuu: Tutahakikisha Wauza Madawa ya Kulevya Wote Wanakamatwa

Serikali imesema kuwa itahakikisha inashughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo vyote vya kisheria vimeagizwa kushirikiana kwa kusimamia sheria ipasavyo.

Hayo yalisemwa jana  Jijini Dar es salaam na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa kongamano linalohusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Alisema kuwa kila mzazi au mlezi aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.

“Ni ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo vinavyopelekea matumizi ya dawa haramu za kulevya,  hivyo ni matarajio yangu kuwa mtaliangalia kwa kina tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo kwa kiasi kikubwa linatuathiri kama Taifa katika mipango ya Serikali na maendeleo ya Taifa letu,” alisema Majaliwa.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii yenye  kuzingatia maadili nchini na Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akisisitiza Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.

Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siang’a aliwaomba viongozi wa dini kuunga mkono Mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa watu wote.

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi alisema viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
Loading...

No comments: