UCHAMBUZI: Kirusi cha ‘WannaCry’ kimeitikisa dunia - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 18, 2017

UCHAMBUZI: Kirusi cha ‘WannaCry’ kimeitikisa dunia

BILL MARWA
BILL MARWA 
By Bill Marwa
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Tanzania ina watumiaji wa intaneti takriban milioni 20. Takwimu zinaonyesha kuna watumiaji wa intaneti wapatao bilioni 3.5 duniani kote.
Wakati matumizi ya intaneti yakizidi kukua kwa kasi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa, huduma na bidhaa mbalimbali mfano malipo kwa njia za simu uhalifu nao unashamiri.
Uwapo wa mitandao umeimarisha biashara na kuongeza mchango kwa uchumi wa mataifa mbalimbali. Kadri dunia inavyozidi kukumbatia mabadiliko ya teknolojia ndivyo changamoto nyingi zinajitokeza hasa waharifu kutokana na mianya mbalimbali iliyopo hivyo kuathiri watumiaji.
Mwishoni mwa wiki iliyopita lilitokea shambulizi la mtandao lililoathiri mifumo ya mashirika, kampuni na taasisi kubwa likiwamo Shirika la Afya Uingereza (NHS) na kusambaa Japan na China pamoja na nchi mbalimbali duniani.
Kirusi kinachoitwa WannaCry au WannaCrypt kilianza kusambaa ulimwenguni kuanzia Ijumaa ya wiki iliyopita na hadi sasa zaidi ya kompyuta 200,000 kutoka zaidi ya nchi 150 zimeathirika.
Kirusi hiki, kinapoingia kwenye kompyuta ya mtumiaji, huyateka na kuyafungia mafaili yote na kutoa ujumbe unaomlazimisha mhusika kulipa Dola 300 za Marekani (zaidi ya Sh660,000) ili yafunguliwe.
Waharifu waliotengeza kirusi huyu humlazimisha mtumiaji kulipa kwa kutumia bitcoi, mfumo wa malipo kwa njia ya dijitali ambao ni ngumu kumfahamu mpokeaji. Kiuhalisia hata ukilipa, sio uhakika wa mafaili yako kufunguliwa.
Kirusi hiki kimeleta madhara kwenye kompyuta zenye mfumo wa kiuendeshaji wa Microsoft Windows na husambaa zaidi kwenye kompyuta ambazo ziko kwenye mtandao au network moja.
Imeripotiwa kwamba uwezekano wa kirusi hiki kufanya kazi uligundulika Machi mwaka huu na Aprili, Kampuni ya Microsoft ilitoa programu maalum ya kuziba mwanya huu lakini ilikua lazima watumiaji waiingize (update) programu hii kwenye kompyuta zao. Walioathirika ni wale ambao hawajafanya hivyo.
Kwa sasa kimezuiwa lakini hili sio jambo la kushangilia sana kwani ni rahisi wahalifu wengine kunakiri programu hii na kuendelea kuisambaza. Ni muhimu kwa watumiaji wote wa vifaa vya kisasa vya kielektroniki kufahamu kila mmoja ana wajibu wa kulinda usalama wake mtandaoni.
Watumiaji wanashauriwa kuzilinda kompyuta zao kwa programu za kisasa za ulinzi ili kuzuia uvamizi wa namna hii. Ikumbukwe, hili huwa halizisaidii kompyuta ambazo zimeshaathiriwa na kirusi hiki.
Watumiaji wa intaneti wanashauriwa kuepuka kupakua mafaili ambayo hawana uhakika wa chanzo chake au kuweka (install) program ambazo hawazitambui. Watumiaji pia waache kubonyeza viunganishi kwenda kwenye tovuti ambazo hazitambuliki au zinazotia shaka.
Wahalifu wengi wa mtandaoni hutumia barua pepe kama njia ya kupenyeza programu zenye virusi, hivyo ni muhimu kwa watumiaji kuwa makini wanapozifungua hasa zenye viambatanisho (attachments) na kuzi-scan kwa program za kuondoa virusi (antivirus) kabla ya kuzipakua.
Pia waepuke kujisajiri kupokea baruapepe kutoka vyanzo ambavyo hawavifahamu. Ni muhimu pia kuwa na sehemu nyingine ya kuhifadhi taarifa (backup) zenye programu za kuondoa virusi zinazofanya kazi wakati wote.
Watumiaji wanashauriwa kuhifadhi taarifa muhimu kama vile majina, tarehe ya kuzaliwa au namba ya vitambulisho mbalimbali kwa umakini. Na wakati wote, kukumbuka kuzingatia sheria na sera za mitandao.
Mwandishi anapatikana kwa namba 0764 568 926.

CHANZO; MWANANCHI

Loading...

No comments: