FEDHA ZINAHITAJIKA HARAKA KUZUIA UPUNGUZWAJI WA MGAO WA CHAKULA KWA WAKAMBIZI WAISHIO NCHINI TANZANIA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, August 28, 2017

FEDHA ZINAHITAJIKA HARAKA KUZUIA UPUNGUZWAJI WA MGAO WA CHAKULA KWA WAKAMBIZI WAISHIO NCHINI TANZANIA
KIGOMA – Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelazimika kupunguza mgao wa chakula kinachotolewa kwa wakimbizi 320,000 wanaoishi katika kambi za Mtendeli, Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma kaskazini magharibi mwa Tanzania kwa sababu ya upungufu wa fedha. WFP inahitaji kwa haraka jumla ya Dola za Marekani milioni 23.6 kuanzia sasa hadi Desemba, 2017 ili imudu kuendelea kutoa mgao unaokidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania.
Shirika la WFP hugawa vyakula vya aina tano tofauti kwa wakimbizi – ambao kimsingi wanatoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Vyakula hivi ni pamoja na unga wa mahindi, kunde, Nafaka Kuu, mafuta ya mbogamboga na chumvi.  Kwa sababu ya upungufu wa fedha, aina zote tano za vyakula kwa mwezi Agosti zinakidhi tu asilimia 62 ya kiasi cha kalori 2,100 zinazopendekezwa kitaalamu kutosha mahitaji ya mtu ya siku.
“Pasipo mwitikio wa haraka kutoka wa wahisani, itakuwa lazima kupunguza mgao kwani akiba ya chakula inapungua kwa kasi sana,” alisema Mwakilishi wa Nchi wa WFP Tanzania Michael Dunford. “Wakati ambapo WFP inashukuru sana kwa msaada uliokwishatolewa hadi sasa, tunatoa wito ili wahisani waitikie haraka na kuwasaidia wakimbizi na kutoa fedha zaidi ili tugawe mgao kamili na kuzuia athari mbaya zisidumu kwa muda mrefu.”
Kupunguza mgao kunasababisha matatizo mengi yanayoweza kubadili vibaya maisha ya wakimbizi. Kupunguza kiasi cha kalori na msaada wa lishe kunaweza kusababisha utapiamlo mkali na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa. 
Licha ya aina hizo tano za vyakula, Shirika la WFP pia hugawa vyakula vya moto kwa wakimbizi mara baada ya kuwasili, mgao wa chakula cha nyongeza kwa wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha na msaada wa chakula kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini na kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI. Hadi sasa vyakula vya moto vinavyogawiwa kwa wakimbizi wanaoingia nchini na programu ya chakula cha nyongeza havijaathiriwa na punguzo la sasa la mgao.
#                      #                      #
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) ndiyo wakala ya kiutu kubwa zaidi linalopambana na njaa kote ulimwenguni, huku likitoa msaada wa chakula katika nyakati za dharura na kushirikiana na jamii ili kuimarisha lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru. Kila mwaka, WFP linatoa msaada kwa watu wapatao milioni 80 katika nchi 80.
Tufuatilie kupitia Twitter: @wfp_tanzania and @wfp_media
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Fizza Moloo, WFP, Fizza.Moloo@wfp.org, simu. +255 (0) 784 720 022 or +255 (0) 759 686 543

Loading...

No comments: