Idara yake ya Uhamiaji yawahakikishia Watanzania kuwachukulia hatua raia wote wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha Sheria - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, August 5, 2017

Idara yake ya Uhamiaji yawahakikishia Watanzania kuwachukulia hatua raia wote wa kigeni wanaoingia nchini kinyume cha SheriaSeeBaitZimekuwepo taarifa za kuingia nchini kwa wahamiaji haramu kupitia mpaka wetu na Nchi ya Kenya. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  kupitia Idara yake ya Uhamiaji inawahakikishia Watanzania kwamba  hatua  kali za kisheria  zinachukuliwa  dhidi  ya raia wote wa kigeni  wanaoingia  nchini kinyume cha  Sheria  za Uhamiaji  na nchi yetu.
Kimsingi hakuna raia  yeyote wa kigeni anayeruhusiwa kuingia nchini kwa kisingizio cha  kuja kufanya kazi, biashara au Uwekezaji bila kufuata Sheria  na taratibu za Uhamiaji, na kwamba  wote wanaokiuka  Sheria hizo watarudishwa makwao mara moja.
Ni jambo lisilokubalika mtu atoke nchini kwake bila kibali cha kufanya kazi Tanzania kwa madai kwamba alishatuma maombi ya kibali husika na amekuja kusubiri majibu ya kibali hicho akiwa Tanzania. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi haitavumilia ukiukwaji huu wa sheria za nchi na kwamba kila raia wa kigeni  anayekusudia kuingia nchini ahakikishe ana kibali cha kuingia nchini na anafanya kazi ambayo ndiyo aliyoiombea kwenye kibali chake.
Yapo matukio ya raia wa nchi jirani, hususan katika mipaka ya Kenya na Uganda ambapo kutokana na hali  ya muingiliano  wa kiuchumi na kijamii, raia  wa nchi zetu, wamekuwa  wakivuka mipaka  pande zote  kufuata huduma mbalimbali, Hii pia inachangiwa na mapungufu katika  usimamizi wa alama na maeneo ya wazi ya mipaka yetu. Hali hii inapelekea baadhi ya wananchi wetu kutumia mwanya huo kuwatengenezea  raia  wa kigeni mazingira ya kuingia nchini bila  kufuata taratibu au hata kutumiwa katika biashara haramu ya kusafirisha  binadamu.
Tahadhari inatolewa kwa Watanzania wote ambao wamekuwa wakiwapokea raia hao  wa kigeni na kuwahifadhi, kwani kufanya hivyo  ni kuvunja  sheria za nchi ikiwemo ile Sheria  ya usafirishaji  haramu wa binadamu.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara yake ya Uhamiaji imeanza kuchukua hatua ili kuweza kushughulikia suala hili. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala, tayari ametembelea baadhi ya maeneo ya mipaka yetu hususani kijiji cha Jasini wilayani Mkinga mkoani Tanga ili kujionea hali halisi na kutoa Maelekezo ya hatua  za kuchukua  kudhibiti hali hiyo kwa mujibu wa Sheria, kwa kuwa eneo hilo linaonyesha kuwa na muingilino baina ya nchi ya Kenya na Tanzania kwa muda mrefu.
Wizara itaendelea na Mashauriano na Mamlaka nyingine zenye dhamana ya Kusimamia alama za mipaka ya nchi yetu kwa kuwa tatizo hili la muingiliano wa wananchi wa pande zote lipo kwenye mipaka mingi ya nchi.
Imetolewa naChristina R. MwangosiKaimu MsemajiWizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi4 Agosti 2017
Loading...

No comments: