Kampuni ya Yussuf Manji kufutiwa leseni na TCRA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, August 18, 2017

Kampuni ya Yussuf Manji kufutiwa leseni na TCRA


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusudio la kufuta leseni ya Kampuni ya Mycell inayomilikiwa na Quality Group Limited (QGL) ambayo imekuwa ikiongozwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji.
Kwa mujibu wa sheria, TCRA iliyoanzishwa mwaka 2003 ina jukumu la kusimamia, kutoa na kufuta leseni za mawasiliano kwa kampuni yoyote ambayo imeshindwa kutekeleza majukumu iliyoyabainisha.
“Kampuni ya Mycell imeshindwa kurekebisha ukiukwaji wa masharti ya leseni,” inasomeka taarifa iliyotolewa na kuwekwa kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.
Kutokana na upungufu huo, “TCRA inauarifu umma kuhusu kusudio la kufuta leseni za Mycell za kujenga miundombinu kitaifa, kutoa huduma kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao na kutumia masafa ya mawasiliano.”
Kuonyesha juhudi ilizochukua kabla ya uamuzi huo, TCRA imesema Januari 27, 2016 ilitoa amri ya utekelezaji kwa kampuni hiyo kwa kukiuka masharti ya leseni walizopewa na kushindwa kutoa huduma kinyume cha Kifungu 21 (a) na (b) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2010.
Hata hivyo, Mycell haimo kwenye orodha ya kampuni zilizopewa leseni na TCRA ambazo zimo kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.
Mamlaka hiyo imeeleza kwenye taarifa yake ya kusudio la kuifuta Mycell kuwa iliipa kampuni hiyo leseni nne tofauti Novemba 21, 2008.
Inafafanua kuwa leseni hizo ni ya kujenga miundombinu kitaifa, kutoa huduma kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao wa mawasiliano na kutumia masafa ya mawasiliano.
Loading...

No comments: