MAKALA ;Utaifa Wetu - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, April 29, 2018

MAKALA ;Utaifa Wetu

Na Costantine Magavilla


Kuna maswali manne ambayo yamekuwa yakiniumiza kichwa baada ya mjadala wa muundo wa serikali kupamba moto kwenye mchakato wa kuunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
1. Kwanza, je utaifa wetu ni nini? Ina maanisha nini mtu kujiita Mtanzania? 
2. Pili, je kuna usahihi kutofautisha dhana ya Utaifa na serikali? Kwa maana kuu moja, katika mijadala ya kisiasa kuna usahihi tukitofautisha au kuweka mipaka kwenye kujadili masuala yanayohusu Taifa hili kukomea kwenye majukumu ya serikali na vyombo vingine vya kitendaji? 
3. Tatu, je Nyerere na Karume wana makosa kwenye hili suala la muungano? Je Karume alikosea kuongoza mapinduzi ya Zanzibar? Je Nyerere alikosea kuungana na jirani yake nchi nyingine huru kuunda nchi moja? 
4. Nne, je tumekosea wapi kama Taifa hadi tunafika sehemu hii tulipo sasa tunahoji Utaifa wetu au tunatoa fursa kwa watu kuhoji dhana ya Utaifa na watu wanakubali kuhoji Utaifa wetu? 
Je Utaifa wetu ni nini?
Nikianza na swali la kwanza linalosema Utaifa wetu ni nini? Tukisema sisi ni Watanzania tunamaanisha nini? Mtu akisema yeye ni Mmarekani inamaanisha nini? Mtu akisema yeye ni Mjerumani au Muingereza inamaanisha nini? Mimi ninaamini katika hili, Utaifa wa nchi hautofautiani na nafsi ya binadamu. Mwanadamu hawezi kujitenganisha na historia yake. Hawezi kuchagua tukio moja na kuliacha lingine katika mjumuisho wa yale mambo yaliyopelekea kumfanya yeye awe vile alivyo. Binadamu aliyekamilika pale alipo ni mjumuisho wa yote yaliyomkuta kuanzia alipoanza kuishi mpaka hapo alipofika yawe mazuri au mabaya. 
Mimi naamini Utaifa wetu hauwezi kutofautishwa na hili. Utanzania wetu hauchagui tukio. Hatujiiti Watanzania kwa sababu ya tukio moja ama matukio mawili au matukio matatu, au matukio kadhaa tukiacha mengine. Tunajiita Watanzania kwa kutambua mjumuisho wa yote yaliyopelekea sisi kufika hapa tulipofika tukawa Watanzania. Na hakuna hata kimoja kati ya vile viliyopelekea sisi kuwa hivi tulivyo tunaweza kuvihoji tukasema hiki sio, hiki ndiyo, hiki hapana, hiki kipo, hiki hakipo. Vyote vinachangia na vina mchango mahususi ambao umepelekea sisi kuwa Watanzania na ni mwongozo wetu ambao ni wa kipekee kama taifa.
Yule ambaye anakataa au anashindwa kuthamini historia yake hawezi kuishi kwa amani na utulivu kwenye mwendelezo wa maisha yake ya mbele. Amani na utulivu vinategemeana sana na mtu kukubali yote yaliyohusika katika maisha yake ya nyuma. Kutokuthamini maisha yako yaliyopita kunachangia kwa asilimia kubwa mtu kutokuwa na amani katika maisha yake ya baadaye. Na mimi ninaamini kama Taifa hatuwezi kuwa na utulivu wa kweli kama hatutakubali kwamba yote yaliyojiri huko nyuma yanatuhusu na ni ya kwetu na sio ya mtu mwingine. Na mataifa yote duniani yaliyokomaa ni mataifa yanayoipa kipaumbele historia ya nchi, sio kuikataa ila kuikubali na kuipa nafasi stahili katika kujumuisha muonekano au ile taswira ya lile taifa. Mengine ni ya aibu na mengine ni ya kujisifu lakini yote yanahusika. 
Sasa mimi ninachokiona pamoja na hayo ni kwamba tukiongelea suala la Utaifa tunaongozwa na imani kuwa Taifa ni dhana kuu ya nchi ndiyo kitu kilicho juu yetu sisi sote. Utaifa ni imani. Hakuna aliye juu ya Utaifa wetu na kila alie anae kiri Utaifa wake lazima awe muumini wa Utaifa huo. Vyombo vyote vilivyoundwa vimeundwa kwa mamlaka yanyotokana na Utaifa wetu. Vyombo hivyo vimeundwa kwa maudhui ya kulinda Utaifa wetu sio tu kwa vizazi vya sasa bali hata kwa vizazi vijavyo. Na viongozi wote wanaokula kiapo wanakula kiapo kwa maana moja kuu, kusimamia na kuulinda Utaifa huu. Mapambano ambayo sisi tunayafanya sasa hivi katika kuleta mabadiliko ya nchi tunayafanya kwa uchungu tulionao na taifa hili la Tanzania. Kiu ya kuona maendeleo ya kweli ndani ya Taifa hili la Tanzania ndiyo yamepelekea mwamko wa kusema tufanye nini Taifa hili lizidi kuimarika. 
Abraham Lincoln ni rais wa Marekani ambae anaheshimika sana na pengine kukubalika kuliko rais mwingini katika historia ya nchi hiyo. Ila Abraham Lincoln ndio rais pekee wa Marekani mwenye sifa ya kusimamia vita ya Wamerikani wenyewe kwa wenyewe. Vita ambayo kwa sasa ni moja kati ya ishara za Utaifa wa Wamerikani. Alifanya hivyo kwa kusimamia Muungano wa Taifa hilo na kutimiza wajibu wake wa kuulinda Utaifa huo. Alikuwa tayari wananchi wafe Taifa lisimame. Taifa ni zaidi ya nafsi.
Je kuna usahihi kutofautisha dhana ya Utaifa na serikali?
Haya yote ambayo yanatupa ujeuri mjini yanatokana na sisi kutambua Taifa hili. Na ndiyo maana ninajiuliza je kwa kutambua hili ni busara kwa Taifa linalosimamia Utaifa wake kuchukulia dhana ya Utaifa kuwa sawa na serikali? Siamini kwamba serikali ni Tanzania, serikali ni ya Tanzania. Kwa maana hiyo siamini kwamba Tanzania ni Chama Chama Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwa serikali iliyo madarakani imeundwa na CCM na serikali ndiyo inayoongoza shughuli ambazo zinatupeleka sisi kimaendeleo lakini yote hayo yanafanyika kwa maana kuu ya kusimamia uendelevu na uimara wa Taifa letu. Sidhani kama ukienda Marekani unaweza kukutana na Mmarekani ambaye anahoji Utaifa wake na bado akakiri Utaifa huo. Mimi ninaamini ukomavu wa kweli katika siasa endelevu ni uwezo wa sisi wananchi na wanasiasa wanaotuongoza kuiwajibisha serikali na sio kuliwajibisha Taifa. 
Tufike hatua tutambue kwamba Taifa kama lilivyo halina uwezo wa kutenda. Kwa hiyo lenyewe kama lilivyo haliwezi likawajibishwa. Taifa halifanyi kitu chochote lenyewe kama lenyewe ndiyo maana aliyewahi kuwa Rais wa Marekani J. F. Kennedy aliwasihi wananchi wake kwamba “Usiulize nchi yako itakufanyia nini bali jiulize utaifanyia nini nchi yako” kwa sababu nchi yetu haiwezi kutufanyia chochote pasipo na utendaji wetu au serikali tuliyoiunda. Kwa hiyo ukomavu wa kweli katika siasa unatutaka sisi tupande mbegu za kuwawezesha Watanzania kuthamini nchi yao, kudhamini Utaifa wao, kuthamini Taifa na kuwa tayari kupambana na yeyote yule ambaye anakwenda tofauti na fikra hiyo.

Lakini ninachoshangaa ni kwamba watu wanachanganya serikali na Taifa halafu mwisho wa siku wanaanza kuhoji vitu mbalimbali ambavyo kwa Mtanzania wa kawaida anaanza sasa kusema yeye ni Mtanganyika? 
Je Nyerere na Karume walikuwa na makosa? 
Mimi ninashangaa sana kuona watu wanamshambulia Nyerere kwenye hili suala la Muungano. Kwa sababu ninavyoamini hata wale wapigania Uhuru wa Afrika kilichokuwa kinawaongoza kabla ya uhuru kupatikana ni muungano wa Afrika. Vuguvugu la muungano wa Afrika lilikuwepo kabla ya nchi za kiafrika kupata uhuru. Nyerere alikuwa ni muumini wa umoja wa Afrika. Na kwa sababu Nyerere alikuwa ni mkweli kwenye hili ni kiongozi pekee aliyepigania Uhuru na baada ya kupata Uhuru wa nchi yake akaendelea kusimamia umoja wa Afrika na mapambano ya Uhuru wa nchi nyingine. Wengine wote baada ya kupata Uhuru wakaishia kuingia mitini. 
Sasa iweje Nyerere tumsifu kwa kumpokea na kumsaidia Mandela, kwa kumsaidia Samora Machel na kuungana nao katika mapambano ya kuwawezesha watu wao kuwa huru, kuwapa hifadhi watu wao hadi kwenye msiba wa Mandela tukapewa heshima ya pekee ila kwenye hili suala la kwenda kwa jirani na kutafuta muungano tunamshangaa. Halafu tunathubutu kusema ni jambo ambalo lilikuwa la kushtusha au pengine la kinyemelea. Kwani Zanzibar hawakuwa na mkandamizaji? Tunamtofautishaje Mzanzibar na Mtanganyika? Huku kulikuwa na mkoloni mwingereza Zanzibar kulikuwa na utawala wa mwarabu. 
Sasa tofauti iko wapi? 
Kwa hiyo maana yake tunasema kwamba Karume kuongoza mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa ni makosa? Yeye kuwa na kiu kwamba wananchi wa asili wa Zanzibar waweze kujitawala wasikandamizwe ni makosa? Halafu Nyerere kutambua kwamba huyu aliyemfukuza ni mtu mwenye nguvu nyingi kwa hiyo kwa kukaa peke yake kunaweza kukahatarisha mazingira ya usalama na kuamua kuungana naye kuimarisha Uhuru na Umoja wa nchi hizo kwa sababu kwa dhamira Afrika ni moja je ni makosa? Kwa mtazamo wangu haya yote yaliendana na tabia ya Nyerere. 
Nyerere alikuwa mwanasiasa mkweli mpenda maendeleo na mthubutu. Na kwa mazingira yale yaliyokuwepo hakika hata ukiangalia sasa hivi hali inavyokwenda unaona dhahiri kilichofanyika kilihitaji uthubutu wa pekee. 
Na sisi kama taifa tukumbuke kwamba vitu vingi vinafanyika na tunatoa dhamana kwa viongozi kwa sababu mtanzania mmoja mmoja hawezi kushiriki katika kila uamuzi. Na ndiyo maana tunafanya chaguzi. Mtanzania mmoja mmoja anashiriki katika jambo hili moja kwa moja kupitia uchaguzi. Akishafanya vile anatoa dhamana kwa vyombo vile husika serikali, bunge n.k. Na kutokana na hali hiyo basi hawa wanaofanya haya maamuzi wana mamlaka, na ndiyo maana ninahoji je Nyerere na Karume wana makosa? Walitumia nafasi walizopewa kikatiba na wakafuata taratibu zote husika za kikatiba kwa sababu walikuwa na mamlaka. 
Leo hii unataka kuniambia kwa mfano mheshimiwa Rais akihudhuria kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa maamuzi yanayofanyika kule huwa tunapiga kura za maoni kwetu Tanzania? Unataka kuniambia Mwingereza wakati anapanua himaya yake kutawala nchi mbalimbali za dunia alikuwa anakwenda kupiga kura za maoni kule kwa Waingereza kuwauliza je twende kule? Si walikuwa wanafanya chini ya mamlaka husika. Sasa kwa nini historia hiyo tunaikubali? Kwanini sisi kama watanzania hatujaukana ujumuiya wa madola? Kwa sababu ujumuiya wa madola ni toleo la matukio ambayo yalitokana na hali ile. 
Kwa nini hatuukani ujumuiya wa madola wetu? Kwanini historia ile tunaikubali ya kwetu tunaikataa? Ndiyo maana nilisisitiza pale mwanzoni kwamba Utaifa wetu ni yote mazuri na mabaya. Tukianza kuchagua chagua ndiyo tunaanza kupata shida. Na tukianza kuchaguachagua hii inakuwa ni tabia yetu sisi watanzania tutakuwa tunachagua chagua kila kukicha na hata haya ambayo yanafanyika sasa huko mbeleni kuna wengine watayaangalia na kuyatafutia makosa, tujadili vyote lakini sio utaifa”
Je tumekosea wapi? 
Nilipata fursa ya kukutana na mtu akaniambia alikuwa na kijana mmoja ambaye anasoma shule ya wafaransa (French School). Huyo kijana alikuwa kwenye dhifa moja akaona bendera ya Ufaransa akaishia kushangilia na kufurahia kuiona ile bendera. Huyu kijana hajawahi kuishi wala kuzuru Ufaransa ila anasoma tu kwenye shule ya wafaransa hapa Dar es salaam. Sio Mfaransa ni Mtanzania lakini kwa mfumo tu ule wa elimu uliopo pale umempa imani na kitu ambacho hata yeye hakijui. Kwenye hili siwezi kuwalaumu Watanzania. Lazima tujiangalie vizuri hasa kwenye upande wa elimu ya msingi. Wakati Nyerere anasimamia hatua za awali za ujenzi wa taifa hili aliwekeza sana kwenye elimu na kuwapa watu fursa waingie kwenye tanuru la elimu na kutumia hiyo njia kama mbinu ya kuwajenga Watanzania. 
Ukienda Marekani wanafunzi wa shule za msingi wanafundishwa na kuaminishwa juu ya Utaifa wao. Wanaaminishwa ingawa Marekani ni taifa ambalo kimantiki halina wazawa. Wamarekani karibia wote asili yao ni ya nje ya Marekani. Lakini wanapitishwa kwenye tanuru hili la elimu wanaaminishwa. Na taifa linahakikisha kuwa kwenye mjadala wa kitaifa vile vitu ambavyo ni miiko haswa vile ambavyo vinagusa Utaifa havipewi fursa. Mimi nashangaa kwa sababu huu mjadala wa katiba mpya hususani kipengele cha muundo wa serikali nikiutazama kwa asilimia fulani unagusa kwenye imani za watu kisiasa. Ninaamini kwenye imani ni vigumu sana kufikia mwafaka. 
Mathalani ukisema wewe bwana ni mkristo, wewe bwana ni muislamu basi tukae tujadiliane tujue kati ya dini hizi mbili ipi ni nzuri zaidi huwezi kufikia mwafaka hata siku moja. Kwa hiyo kuna mijadala ambayo haipewi nafasi hatakama watu wapo ambao wangependa kuijadili wapo kwa sababu mwisho wake kila siku ni kupanda mbegu za chuki na utenganifu. Kupanda maswali ambayo mwisho wa siku hayana majibu yana mitazamo. Mwishowe tunafankiwa kuwalisha watu sumu ya utengano ya kufikiria ‘umimi’, na ‘usisi’.  
Mimi ninafurahia sana kuona matukio mazuri ambayo yanaweza kuchangia kuwahamasisha wananchi, nyimbo za kujumuisha watu, matukio ya kusheherekea umoja wetu, lakini ninaamini msingi imara wa taifa letu utajengwa na elimu inayozingatia jukumu hilo la kumjenga Mtanzania. Mtu ambaye atapambana kwa nguvu zake zote kutetea Taifa letu sio kuligawa. Mtu ambaye anatambua kwamba serikali ni chombo kinachofanya kazi ya kusimamia maslahi ya wananchi mbele ya Taifa lao ila serikali sio Tanzania. Kwa hiyo serikali kukosea haimaniiishi kwamba Tanzania ina makosa. Tusitumie mwanya huu wa kuunda katiba mpya na kuigeuza kama fursa ya kuitolea uvivu CCM na serikali yake hata kwa kuuweka rehani Utaifa wetu.
Mwisho wa siku tukichanganya mambo mtu anakata tamaa sio tu na CCM na serikali yake bali anakata tamaa hata na Taifa hili ambalo bado linahitaji utetezi. Sasa ninawashangaa hawa ambao wanatumia nguvu nyingi kuwachanganya watanzania ambao tayari hawaelewi kuwa pengine serikali na Taifa si kitu kimoja. 
Hatuwezi kuingiza siasa kwenye Utaifa. Siasa ni kwenye serikali, siasa ni kwenye bunge, siasa ni kwenye vyombo vile husika ambavyo vinatumika kulinda Taifa lakini sio kwenye Utaifa wetu. Kwa sababu tunavyochokonoa taifa letu tunawapa fursa maadui zetu wa nje mwanya wa kutuona kuwa sisi ni wadhaifu na hatuna umoja wa kweli. Kwa hiyo hapo tunakuwa tunapata kitu kingine kabisa ambacho kinaelekea kwenye uhaini. Kwa nini tutoe nafasi kwa Tanzania kuoneka dhaifu?   

UTAIFA NA VIJANA
Mimi ni mwanaharakati kwa asili na ni mwanaharakati ambaye ninapenda sana maendeleo ya nchi yetu. Ninapenda sana maendeleo ya Watanzania na ninaamini sana maendeleo ya nchi yatategemeana na Watanzania kujiaminisha katika uwezo wao wa kuchangia katika maendeleo hayo. Katika hatua za awali kabisa za utambuzi na ufahamu wangu na kujua kwamba Watanzania wapo wengi wenye nia lakini wanakosa fursa kwa sababu wanabezwa na mwongozo wa jumla jumla, mjumuisho wa kimawazo ambao kwa zaidi unaturubuni. Tukae tukijua kuna watu wanawekeza katika kuturubuni, nitakupa mfano mdogo tu hususani “maana ya Ujamaa”. Kati ya vitu ambavyo vinapotoshwa na vinapotosha ni dhana ya “Ujamaa” na mchango wake kwa Tanzania ya leo. 
Mimi ninafikiri Ujamaa (kama mpango/mfumo wa maendeleo) unadhihirisha uwezo wa kiongozi kufanikisha mpango anaoutaka yeye angalau kwa maana ya kuutekeleza hata kama hautakuwa na ufanisi na sio kuishia kwenye kutafuta wa kumlaumu. Lakini lazima tutambue ukweli kwamba Ujamaa ulidumu kwa miaka si zaidi ya tisa katika historia yetu ya miaka hamsini. Azimio la Arusha lilikuwa mwaka 1977 na Nyerere aling’atuka madarakani mwaka 1985. Kwa hiyo tunapofika mwaka 2015 tuna miaka thelathini bila Ujamaa tukifananisha na miaka tisa ya Ujamaa. Ila mpaka leo kuna viongozi wanathubutu kusimama na kuwarubuni Watanzania kwamba sisi maendeleo yetu yanachelewa kwa sababu ya Ujamaa. Kwani Nyerere alishindwa kusimama kwenye jukwaa na kusema maendeleo yatachelewa kwa sababu ya ukoloni?
Viongozi kwa kukosa uthubutu na ubunifu wa uwezo wa kupangilia mambo yao wanamlaumu Nyerere na Ujamaa wake ambao ulikufa mwaka 1985. Na baada ya pale kila mmoja akawa na fursa ya kufanya la kwake kwa sababau Mwalimu hakuwa mtu wa namna hiyo na naamini kabisa ukiongea na Rais wa awamu ya pili alifanya yake, na aliyekuja baada ya hapo naye atakiri alifanya yake. Sasa iweje sasa hivi tuendelee kumlaumu Nyerere na Ujamaa wake baada ya miaka thelathini? 
Je, kuna mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba mwaka wa elfu mbili na kumi na nne ambaye alisoma kipindi cha Ujamaa wa Nyerere? Kuna mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba mwaka wa elfu mbili na kumi na nne aliyesoma kipindi cha miaka kumi baada ya Ujamaa wa Nyerere? Kuna mwanafunzi aliyesoma akamaliza mwaka wa elfu mbili na kumi na nne darasa la saba aliyesoma kipindi cha miaka ishirini baaada ya Ujamaa wa Nyerere? Kuendelea kuulaumu Ujamaa ni urubunifu. 
Sisi kipindi kile kwa kutambua haya, kwamba tuko katika Taifa la kulaumulaumu na sio Taifa la kuchochea na kusimamia maendeleo na tukasema tuwape watu, haswa vijana, changamoto ya kufanya hivyo. Bahati nzuri mimi nikakutana na vijana wengine ambao wao walikuwa na mawazo sawa na ya kwangu na pengine walinitangulia kwa sababu ndiyo tukisema ni waasisi wao ndiyo walikuwa ni waasisi kweli. Vijana ambao walisimamia wakaanzisha “ROOTS AND SHOOTS” na baadaye ndiyo tukaanzisha na haya mambo ya YUNA na TYVA. Tulikuwa wote na mawazo sawa na kikubwa tulichokifanya ni kuwaaminia vijana wenzetu kwamba tunaweza.  
Hatukuchochea sera fulani fulani za kisiasa hata kidogo, tuliwapa watu fursa ya kujiaminisha katika yale maeneo wanayoona yanafaaa wao kukumbatia, sera ambazo zinawafaa wao. Kwa sababu ndiyo madhumuni ya Ujana, kijana asimamie yake ili aweze kufika anakotaka yeye na tulifanikiwa. 
Leo hii tukiongelea viongozi vijana huwezi kuongelea viongozi vinara vijana kumi ukose ambao wanaohusika na vijana wetu sisi wa YUNA na TYVA. Sasa kwa juhudi zile za msingi sisi tuliona mafanikio au matunda yake na ndiyo maana mpaka kesho kutwa mimi ninaamini katika hili. Ninaamini kwamba siasa ina nafasi yake hasa kwenye kuweka wazi mapungufu ya kiutendaji ambayo yanatupeleka sisi kushindwa kufanya yale ambayo yanatakiwa kufanyika ili tupate maendeleo. Lakini mimi ni kati ya wale ambao wanaoamini kazi iliyofanywa na Nyerere ilikuwa sio bure na watu wanaomtuhumu kwa kutupotosha kutuchelewesha hawaelewi msingi imara ya Utaifa unajengwa vipi. 
Tukichukulia mfano wa Marekani. Marekani ni nchi ambayo sisi kwa jicho la mbali tunaiona ni ina mambo mengi, mengine yenye kuonekana yana malengo na mengi yanaonekana kuangamiza zaidi. Lakini Marekani ni nchi ambayo kama Taifa imesimamia misingi thabiti. Wamarekani wanasimamia misingi kama kuthamini ukweli ambayo ni endelevu inayoongoza Taifa lao na hiyo misingi iliwachukua zaidi ya miaka mia mbili kuijenga. Nyerere aliifanya hiyo kazi ndani ya miaka ishirini na tano ya utawala wake, kwa sababu dhamira yake ilikuwa ni ya ukweli. Alitamani kumjenga Mtanzania, alitamani kuijenga Tanzania hakutaka kumjenga Magavilla hakutaka kumjenga Swalehe alitamani kumjenga Mtanzania. Leo hii mikakati inalenga kumjenga Magavilla, kumjenga fulani na fulani lakini Mtanzania yuko wapi? Elimu ambayo inalenga kutotoa watu kwa misingi ya kushiriki tu kwenye mafunzo na sio kwa misingi ya kuelimika kupitia kwenye mafunzo mimi ninaona hapo kuna dosari kubwa kama sio janga. 
Kama Mungu si athumani, tutayaona ndani ya uhai wetu madhara ya kutokujali msingi imara wa elimu ambao unalenga kumjenga Mtanzania mpenda nchi kabla ya nafsi, Mtanzania mzalendo. 
Ninasema hivi kwa sababu umasikini ni kitu kibaya. Na sio umaskini wa pesa ninao uzungumzia hapa. Kuna siku nilikutana na kijana mmoja akaniomba nimsaidie kumtafutia kazi pengine kwa kutambua nafasi yangu akaniambia “Blaza naomba unisaide kunitafutia kazi”. Nikamkubalia na kumuuliza amesoma hadi kiwango gani, akaniambia “Mimi nina elimu ya Manzese”. Nikapigwa na butwaa na kumuuliza “elimu ya Manzese!” unamaanisha nini? akanijibu, “Blaza, Manzese tunaishia darasa la saba”
Enzi zetu sisi, na sisemi hivyo kwa sababu mimi ni mzee sana bali hii ni ishara kwamba historia inakwenda kwa kasi. Ulikuwa ukienda shule kama Shule ya Msingi ya Mbuyuni pale Dar es Salaam unakutana na kila aina ya Mtanzania: masikini, tajiri, mwenye madaraka, mtumishi, aliyeokoka, aliyetukuka, kila aina ya Mtanzania bila kujali uwezo unakutana naye. Kufaulu kwako ni juhudi zako binafsi haijalishi wewe umetokea wapi unaishi wapi, ndugu yako ni nani ni juhudi zako binafsi tu. Na ndiyo maana unakuta kuna Watanzania wengi wametoka kimaisha kwenye mazingira magumu leo hii wanahesabika vizuri kabisa kijamii. 
Kwa hiyo ikifikia hatua watu wa sehemu fulani wanaishia darasa la saba kwa feli au kutokuwa na uwezo wa kuendelea, sasa hapo utasema kweli ni hao watu wenye makosa? Kwamba watu wa sehemu hii wana tofauti gani kiasi cha kusema hawastahili kufaulu? Je, wana mapungufu, wana kasoro? Halafu mwisho wa siku tunakuja kuwakejeli na kuwashutumu kwamba hawa wanafanya mzaha katika masomo. 
Hakuna elimu ya namna hii duniani inayoishia kujenga. Ni elimu ya kibaguzi ambayo inajenga matabaka ya kijamii ambayo mwisho wa siku yanatuletea shida kwa sababu ya kitu hiki kinachoitwa umasikini haswa ule unaotokana na watu kutojitambua na kujiaminisha kwa hicho wanachokitambua. Masikini wa kujitambua na kujiaminisha kwa tabia kila siku anatafuta wa kumlaumu. Tumpe mtu uwezo wa kujitambua. Awe ni masikini wa pesa lakini sio masikini wa utambuzi. Ajitambue na akubali jukumu la kuweza kusimamia maisha yake mbele ya yote haya ambayo yanayoonekana mbele yetu. Sasa hata hiyo silaha ya msingi kabisa ya utambuzi unamkosesha mtu kweli kuna uhai hapo? Kuna Mtanzania hapo? Tuwekeze kwenye elimu inayojenga utambuzi wa nafsi, utambuzi wa Taifa na utambuzi wa kuwa Taifa ni zaidi ya nafsi.  
UTAIFA NA NYERERE
Nyerere anakumbukwa zaidi na watanzania wengi wa kizazi cha sasa kwa matukio yale ya miaka ya tisini kwenda mbele. Haswa pale aliposimama na kukemea serikali ya awamu ya pili, watanzania ndiyo wakatambua kwamba kweli alilipenda Taifa hili zaidi ya hata nafsi. Alivyojiweka mbele ya hatari kusimamia maslahi ya walio wengi Watanzania wanyonge na hapo ndipo unapata taswira kamili huyu mtu alikuwa ni mtu mwenye dhamira gani. Kwamba huyu hakukaa kwenye kile kiti cha urais kwa ajili ya kujijengea mazingira au kumjengea mazingira mtu fulani au kwa ajili ya kufanya hiki au kufanya kile. 
Yale yote aliyokuwa anayabuni yalikuwa yanamlenga Mtanzania, jinsi ya kumsaidia Mtanzania wa kawaida aweze kufanikisha maisha yake. Na kama alipungukiwa, kama binadamu mwingine, alipungukiwa kimawazo. Ni wazi kuwa Nyerere alikuwa ni mwanasosiolojia, amesoma elimu ya jamii na hakuwa mchumi wa kubobea. Mimi mwenyewe ni mwanamasoko nimesomea na nimebobea katika masuala ya masoko na biashara. Pamoja na kusomea sijabobea katika usimamizi wa fedha. Kwa hiyo hata nikipewa uongozi leo kuna vingine nitakuwa ninavifanya kwa kuegemea upande wangu. 
Hayo sio makosa ni mapungufu na hakuna binadamu aliyekamilika. Kila binadamu ana mapungufu yake lakini mimi nikiangalia na kujiuliza kiongozi gani wa kisiasa wa Tanzania hii alikuwa mkweli kabisa amesimama na amesimamia maslahi ya Watanzania kwa dhati sio kwa maana hii ni kazi yangu niifanye, sio kwa maana fulani kanihimiza ngoja niendelee, bali kwa maana ya kukaa na kufikiria Mtanzania anahitaji nini tukimfanyia ataweza kujisimamia, ninaungana na Watanzania walio wengi na kusema kwa sauti moja Nyerere alikuwa mtu wa namna hiyo. 
Kwa bahati mbaya ujamaa Ulienda tofauti na wabaya wake Nyerere wameelemea kwenye Ujamaa na kumuoanisha na Ujamaa utafikiri Nyerere kazi aliyoifanya pekee Tanzania ni kusimamia Ujamaa.  Na ndiyo maana Mungu aliona isiwe taabu, miaka ya tisini akampa nguvu na ujasiri wa kusimamia haki na kuwadhihirishia Watanzania kuwa yeye alikuwa kweli ni Baba wa Taifa na baba kamwe hatamtakia mwanaye njaa. Na ndiyo maana hata ukiongea na Watanzania walio wengi leo hii ambao wanamjua Nyerere, walio wengi leo hii wanamjua Nyerere wa miaka ya tisini. 
Nyerere aliyekuwa anasimamia haki. Nyerere aliyekuwa na uthubutu. Nyerere mwenye kujali. Sasa mtu wa namna hiyo mimi kwangu atakachokisema nitakipa kipaumbele kuliko wengi ninaowaona kwenye siasa sasa kwa sababu najua huyu akisema hawezi kusema kwa mfichomficho. Kwa sababu hata kama anafanya kwa mfichomficho anafanya kwa dhamira ile ya msingi ambayo inatutaka sisi wote tuendelee mbele kama Taifa moja. Na wanaojaribu kumfanya Nyerere aonekane tofauti mimi naamini wao ndiyo waangaliwe upya. Ninayasema haya sio kwa sababu Nyerere hakuwa na mapungufu yake, alikuwa na mapungufu yake lakini sisi Watanzania tukubali kasumba tulionayo. Tuna kasumba ya kudharau na kupuuza vya kwetu. 
Nyerere alikuwa ni mtu ambaye alilenga kuweka msingi nchi ionekane kama ni nchi kamili na sio genge tu la hovyohovyo la watu kupita na kuzunguka. Na ndiyo maana leo hii mtu mwenye dhamira kweli akisimama akifanya kitu cha maana Tanzania kinaitika kwa sababu mfumo wote wa Tanzania umejenga watu waelewa, watu ambao wanapenda maendeleo, watu ambao wanajali utu.
Na ndiyo maana nilisema pale awali kwamba ambaye hathamini ya nyuma atakosa amani kwenye yanayomjia huko mbeleni. Nyerere alikuwa ni mtu wa kukumbukwa kwa yale mema na yale mema ambayo yanamhusu ni yale ambayo yalitujumuisha sisi kama Watanzania, kutufanya tuthamini ubinadamu na kutambua kuwa umoja wetu ndiyo nguvu yetu. Kwa sababu kama wewe ni mzazi kwa mfano; utatambua vizuri sana mtoto anayelelewa kwa kupewapewa pesa tofauti yake na yule ambaye analelewa kwa kuthaminishwa utu.  
Hatuna haja ya kwenda mbali. Watanzania tunalaumu kunyimwa fursa ya kuwa na pesa lakini ambao wangekuwa na hizo pesa ni akina nani kama hizi kasi za kusaka pesa zingeanza wakati ule wa Uhuru? Kwa nchi ambayo ilikuwa haina hata wasomi na umikishwaji ulitegemea asili nani angeishia kuwa na hizo pesa? Kazi ya kujenga msingi si ndogo, si rahisi inahitaji uimara, inahitaji kujiamini, inahitaji uthubutu, inahitaji kujinyima na hiyo kazi aliifanya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambagare Nyerere kwa uweledi, uadilifu na ufanisi mkubwa. Na mimi naamini kama kweli sisi Watanzania ni watu waelewa tutamkumbuka kwa hilo na kumwacha alale mahali pema peponi.


SOMA ZAIDI;http://www.magavilla.com/
Loading...

No comments: