Uwanja wa ndege za kivita wa Syria washambuliwa kwa makombora - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, April 9, 2018

Uwanja wa ndege za kivita wa Syria washambuliwa kwa makombora

Vyombo vya habari nchini Syria zimeripoti vifo vya watu kadha katika uwanja mmoja wa Ndege wa kijeshi nchini humo baada ya shambulio la kutumia Makombora.

Shirika la serikali la SANA limesema makombora kadhaa yalirushwa uwanja wa ndege wa Tayfur, ambao pia hufahamika kama T4 karibu na mji wa Homs, mapema leo Jumatatu.

Shambulio hilo limetekelezwa huku jamii ya kimataifa ikiendelea kulaani shambulio la kemikali ambalo lilitekelezwa katika mji wa Douma ambao unashikiliwa na waasi.

Rais wa Marekani Donald Trump alimweleza Rais wa Syria kama "mnyama" Jumapili na kuonya kwamba yeye pamoja na washirika wake Iran na Urusi "watalipa mauaji hayo".

Bw Trump na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walitoa taarifa siku hiyo na kuapa "kuchukua hatua kali na ya pamoja" kuhusiana na shambulio hilo.

Lakini maafisa wa Marekani wamekanusha uwezekano kwamba Marekani ndiyo iliyotekeleza shambulio hilo.

"Kwa sasa, Wizara ya Ulinzi haitekelezi mashambulio yoyote ya angani Syria," Pentagon imesema kupitia taarifa.

Aprili mwaka 2017, Marekani ilirusha makombora 59 aina ya Tomahawk katika uwanja wa ndege za kivita wa Shayrat nchini Syria baada ya shambulio la kemikali kutekelezwa katika mji wa Khan Sheikhoun uliokuwa unashikiliwa na waasi.
Loading...

No comments: