Afya: Madhara ya kunywa pombe wakati unatumia dawa - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, May 20, 2018

Afya: Madhara ya kunywa pombe wakati unatumia dawa


Mara nyingi wahudumu wa afya tunaulizwa na wagonjwa wakati tunawapa dawa na matibabu mengine kama wanaweza kunywa pombe
au la huku wakiendelea na matibabu.
Swali hilo hufikirisha sana, hususan kwa dawa za muda mfupi na wagonjwa wenye maradhi makubwa.
Mara nyingi tunawashauri wasitumie pombe na tunashukuru kwamba wanaelewa. Sasa swali kwako: vipi ukiacha kunywa pombe kwa muda wakati upo kwenye matibabu? Unaweza ukajibu kupitia barua pepe said.r@afyazaidi.org au simu namba 0784082847.
Mimi sinywi pombe, kwa hiyo ukijibu utanisaidia sana kupata picha ya upande wa pili yaani watumiaji wa dawa ambao wanakunywa pombe.
Pombe ni kemikali na pia ni dawa. Hii huweza kusababisha kuingiliana na kemikali zingine zikiwamo dawa. Muingiliano kati ya pombe na dawa huweza kuleta athari mbalimbali zenye hatari ndogo na kubwa.
Pombe hufanya kazi katika mfumo wa fahamu wa kati (ubongo) na kuingilia ufanyaji wake wa kazi. Pombe hupunguza ufanyaji kazi wa mfumo wa fahamu na kusababisha kusinzia au kulala, kupunguza uwezo wa kufikiria na kukumbuka, kuathiri mfumo wa upumuaji, kuathiri mfumo wa utoaji taka mwili na kuathiri mfumo wa chakula.
Pia, pombe huathiri ufanyaji kazi wa ini na figo na huchangia kuharibu viungo hivyo.
Kama kemikali, pombe huweza kuingiliana na dawa na kuzalisha kemikali nyingine au matokeo mengine ambayo huweza kuwa hatari kwa afya yako.
Huweza kusababisha maumivu makali ya tumbo, usingizi mzito, kuharibu zaidi figo na ini, kuzuia dawa isifanye kazi na kukojoa zaidi.
Pombe pia huweza kukusahaulisha muda wa kunywa dawa au kukupita wakati umelala kwa sababu ya pombe, kukufanya upuuzie dawa na hata kukufanya uache kunywa dawa ili unywe pombe kwa amani. Pia, pombe huweza kuchangia kupunguza ulaji wa mgonjwa na hivyo kuathiri afya na ufanisi wa dawa.
Hadi sasa duniani tuna dawa nyingi na bado wanasayansi wanaendelea kutengeneza nyingine kila siku.
Ukweli ni kwamba, siyo dawa zote huweza kuingiliana na pombe. Dawa nyingine haziingiliani kabisa na pombe na unaweza ukanywa huku unaendelea na dozi zako.
Dawa zinazoingiliana na pombe ni zile zinazoweza kuungana na pombe na kutengeneza kemikali hatari kwa mwili na kuweza kusababisha
madhara kwa uhai au viungo vya mwili. Zipo nyingi sana, endelea kusoma. Dawa zingine zinazoingiliana na pombe ni zile ambazo ufanyaji kazi wake na athari zake huweza kuongezwa au kupunguzwa na pombe.
Mara zote pata ushauri kutoka kwa mfamasia anayekupa dawa au daktari wakati anakuandikia dawa. Atakuambia na kukupa maelezo zaidi kuhusu muingiliano kati ya hizo dawa zako na pombe.
Dawa zisizoingiliana na pombe ni zile ambazo haziwezi kuungana na pombe kwa namna yoyote kikemia na hata kwenye ufanyaji wake wa
kazi na athari zake haziwezi kuathiriana.
Mfamasia au daktari atakuambia na kukupa maelezo zaidi kuhusu muingiliano kati ya hizo dawa na pombe kama u-mnywaji.
Kwanini usitumie pombe wakati unatumia dawa? Sababu kubwa ni kukuepusha na madhara yote yanayoweza kutokana
na pombe.Chanzo: MWANANCHI
Loading...

No comments: