Iran yaendelea kupinga masharti ya Marekani - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 24, 2018

Iran yaendelea kupinga masharti ya Marekani


Iran imeendelea kupinga masharti kutoka Marekani ya kufanyia mabadiliko sera yake ya kigeni na mpango wake wa nyuklia huku mshirika wake Syria, ikitupilia mbali wito wa Marekani kuviondoa vikosi vya Iran nchini humo.

Ufaransa, mmoja ya mataifa yenye nguvu barani Ulaya, iliosikitishwa na hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba wa nyuklia uliyotiwa saini mwaka 2015, imesema hatua ya Marekani ya kuiongezea vikwazo zaidi Iran, itawaimarisha zaidi wanasiasa wenye msimamo mkali nchini Iran.

Jumatatu wiki hii waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo aliitishia iran kuwa itakabiliwa na vikwazo zaidi katika historia iwapo haitaachana na ushawishi wake wa kikanda, akiishutumu nchi hiyo kuunga mkono makundi ya silaha katika mataifa kama vile Syria Lebanon na Yemen.

Pompeo aliyasema haya wiki mbili baada ya rais Trump kujiondoa katika mpango wa kimataifa wa nyuklia wa Iran, uliopelekea taifa hilo kuondolewa vikwazo kufuatia hatua yake ya kukubali kusitisha uendelezaji wa mpango huo. 
Mataifa yenye nguvu barani Ulaya yanauona mkataba huo kama nafasi nzuri ya kuizuwia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Pompeo amerejelea shutuma za zamani dhidi ya nchi yake ila safari hii shutuma hizo zimetolewa kwa ukali zaidi. 

Naye afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran Meja jenerali Mohammad Bagheri, amesema Iran haitaisujudia Marekani katika shinikizo lake la kudhibiti shughuli zake za kijeshi. 
Mjini Paris, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya Marekani kujiondoa katika mkataba huo wa nyuklia na kuiwekea Iran vikwazo itazidisha misimamo mikali na kuhatarisha eneo hilo.

Le Drian amesema Ufaransa itaendelea kutekeleza makubaliano ya mkataba huo hata kama inakubaliana na Marekani kwamba shughuli za nyuklia za Iran pamoja na makombora  zinapaswa kudhibitiwa.

Huku hayo yakiarifiwa Syria imetupilia mbali wito wa Marekani wa kuviondoa vikosi vya Iran nchini humo. Katika vita vya Syria vilivyodumu miaka 7, Iran imekuwa ikitoa msaada muhimu kwa  jeshi la serikali ya Bashar al Assad.
Loading...

No comments: