Mtumbwi wazama, wanafunzi wawili wafariki dunia


Wanafunzi wawili wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wanatumia kuvuka kupinduka na kuzama eneo la Chulwi kitongoji cha Tambani Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani jana Mei 14, 2018. Katika ajali hiyo, watu wanane waliokolewa.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga amesema  leo Mei 15, 2018 kuwa mtumbwi huo ulikuwa na watu 10, wakiwamo wanafunzi hao, kwamba mwili wa mwanafunzi mmoja umepatikana na mwingine unaendelea kutafutwa.

“Wanafunzi hawa mmoja alikuwa anasoma darasa la awali na mwingine darasa la pili,” amesema Sanga.

Amesema kutokana na mvua kuendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani humo, amezuia wanafunzi kwenda shule kwa kuwa pia mito imejaa maji jambo linalosababisha uvukaji kuwa mgumu.

Amesema kuwa mvua hizo zilimfanya ashindwe kufika eneo la tukio jana baada ya gari yake kukwama na amehakikisha leo kufika maeneo yote ambayo yamepata madhara ya mvua.

“Leo nitatembelea maeneo yaliyopata madhara ya mvua eneo la Magawa, Kata ya Kisiju huko kuna nyumba zimeezuliwa na idadi kamili nitatoa baadaye,” amesema Sanga.

Post a Comment

0 Comments