Muuguzi auawa na mumewe, atumbukizwa shimoni - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, May 26, 2018

Muuguzi auawa na mumewe, atumbukizwa shimoni





Mkuranga. Muuguzi Mfawidhi Msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Rosemary Magombora (43) anadaiwa kupigwa na mume wake hadi kufa na kisha mwili wake kufukiwa katika shimo lililo jirani na nyumba yao.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyotolewa leo Mei 25, tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Mkwalia, Tarafa ya Mkuranga wilayani humo na kwamba chanzo cha mauaji hayo inadaiwa kuwa mume wa muuguzi huyo ameambukizwa virusi vya Ukimwi na Rosemary.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Dk Stephen Mwandambo amesema mwanamke huyo alikuwa mtumishi wa hospitali hiyo na kwamba, mara ya mwisho aliingia kazini Ijumaa iliyopita.
"Ni kweli huyu ni mtumishi wa hapa na mimi binafsi nilionana naye Ijumaa iliyopita akiwa kazini, tumesikitika mno kusikia amepatwa na hili tukio la kinyama," amesema Dk Mwandambo.
Dk Mwandambo amesema mwili wa marehemu ulifikishwa hospitali hapo  leo mchana  saa tisa kwa ajili ya uchunguzi  na wakati wowote utakabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.
Akifafanua kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Mohamed Likwata amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Rosemary alipigwa kichwani kwa kutumia rungu na mume mnamo Machi 21 mwaka huu.
“Baada ya kufanya mauaji hayo aliuzika mwili kwenye shimo lenye kina kirefu cha futi saba na nusu,” amesema.
Alisema siku hiyohiyo usiku wa Mei 21, mume wa Rosemary alifika kituo cha polisi na kueleza kuwa mke wake hajarudi nyumbani tangu jana usiku.
“Huyu mtuhumiwa alisema amemtafuta mke wake kwa njia mbalimbali ikiwamo simu bila mafanikio,” amesema kamanda.
Kamanda Likwata ameongeza kuwa mtuhumiwa aliendelea kudai kuwa anahofia mke wake atakuwa amepotea na hivyo amefika hapo kutoa taarifa.
“Kama ilivyo ada yetu timu maalumu ya askari walianza msako huku wakipeleleza na walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa walifanya upekuzi wa kina maeneo yote na kutilia shaka tukio hilo,” amesema.
Likwata amesema Mei 25 ndipo walipojiridhisha kuwa kuna mwili wa binadamu umetumbukizwa katika hilo shimo na kuanza taratibu za kuufukua.
"Tulipojiridhisha kuna mwili wa binadamu tulifanya utaratibu wa kuomba kibali mahakamani ili tuufukue tujiridhishe kama ni wa muuguzi huyo au ni mtu mwingine, na saa tisa alasiri tuliufukua na tukathibitisha ni yeye,”amesema.
Kamanda Likwata amesema mtuhumiwa ameshakamatwa na uchunguzi unaendelea.
Loading...

No comments: