Rais Magufuli aagiza Bilioni 2 za ujenzi wa mabweni UDSM ziende SUA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, May 8, 2018

Rais Magufuli aagiza Bilioni 2 za ujenzi wa mabweni UDSM ziende SUA


Rais John Magufuli ameagiza pesa kiasi cha Tsh. Bilioni 2, za miradi ya maendeleo katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2018/19 zilizokuwa zimepangwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupelekwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), zihamishwe na zipelekwa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) cha Mjini Morogoro.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo kwa Waziri anayehusika na wizara hiyo, Prof. Joyce Ndalichako, leo Mei 7, 2018 wakati akihutubia Jumuia ya Chuo hicho alipokitembelea na kupata fursa ya kusikiliza kero za wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wengine wa chuo hicho ambapo alizitolea ufafanuzi na nyingine kuagiza uongozi wa chuo kuzitatua.

“Mimi ninaamini Chuo Kikuu hiki cha SUA kinaweza kikawa chanzo kikubwa cha kubadilisha maisha ya Watanzania wengi, ninakipenda chuo hiki, si kwa sababu ya jina la Sokoine, ni kwa sababu ya jinsi kinavyofanya kazi.

“Ninafahamu kuwa mna changamoto nyingi, Waziri wa Elimu (Prof. Ndalichako) amesema ametenga Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuongeza majengo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mimi ninasema hizo bilioni mbili haziendi UDSM, nazihamishia hapa ili zianze kujenga mabweni.

“Tatizo langu mimi ni moja tu, ni usimamizi, nimeenda Chuo cha Mkwawa, Iringa, nilikuwa discouraged, ninapotoa pesa ninafuatilia, mimi siyo ‘kilaza’ kwa kufuatilia, ninafuatilia kila senti, na ninafahamu thamani ya pesa.

“Sipendi nitakapokuja hapa SUA halafu nikute hizo pesa zimetumika vibaya. Niwaambie tu ukweli sitaki kuonekana mnafiki, mzitumie vizuri. Mimi ninataka dhamira ile ya Baba wa Taifa aliyeanzisha chuo hiki cha SUA tuienzi kwa dhati na kwa vitendo katika awamu hii ya tano.

“Serikali inatamani hata kujenga mabweni ya wanafunzi wote elfu tisa hapa SUA, lakini wapo tu watakaotoka na kukaa huko (nje ya chuo), unakuta mwingine labda ameoa au ameolewa, lakini nitajenga tu,” alisema Magufuli.

Loading...

No comments: