Serikali Gabon Yajiuzulu kwa Amri ya Mahakama - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, May 3, 2018

Serikali Gabon Yajiuzulu kwa Amri ya Mahakama


Serikali Gabon Yajiuzulu kwa Amri ya Mahakama
Serikali ya Gabon imejiuzulu siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kuamuru Bunge livunjwe na kuagiza uongozi wa nchi ujiuzulu kutokana na kuchelewa kuitisha uchaguzi mkuu.

Taarifa ya Serikali inasema Waziri Mkuu Emmanuel Issoze Ngondet "aliwasilisha barua ya kujiuzulu kutoka nafasi yake serikalini baada ya uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuamuru shughuli za Bunge zisimame hatua iliyolazimisha Serikali kujiuzulu."

Kwa mujibu wa Mahakama Serikali ilipaswa kuandaa uchaguzi lakini uliahirishwa mara mbili kufikia Aprili 30.

Mahakama imesema shughuli za Bunge lililovunjwa sasa zitahamishiwa kwenye Baraza la Seneti hadi uchaguzi mpya ufanyike. Tarehe ya uchaguzi haijatangazwa.

Uchaguzi mkuu ulifanyika mwaka 2016 ambao Rais Ali Bongo alitangazwa kuwa mshindi matokeo yaliyopingwa na upinzani.

Ghasia zilizuka siku chache baada ya uchaguzi na wapinzani wanasema watu zaidi ya 50 waliuawa katika mapigano. Taarifa rasmi ya vifo ni watu watatu.

Bongo alitwaa mamlaka kutoka kwa baba yake Omar Bongo, ambaye alitawala kwa miaka 41 hadi alipofariki dunia mwaka 2009.
Loading...

No comments: