TRA yakomba fedha zote akaunti ya StarTimes ikidaiwa kodi - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Tuesday, May 1, 2018

TRA yakomba fedha zote akaunti ya StarTimes ikidaiwa kodi


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imechukua fedha zote zilizokuwapo katika akaunti ya kampuni ya StarTimes Tanzania kufidia deni la kodi.

Kampuni ya StarTimes iliyoleta mapinduzi ya matangazo ya digitali nchini tangu kuzimwa kwa mitambo ya analogia kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2012, inajishughulisha na uuzaji wa ving’amuzi na vifurushi vyake, simu za mkononi na runinga.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana kwamba mamlaka hiyo imezuia akaunti ya StarTimes kwa sababu ya kushindwa kulipa kodi kwa wakati.

Kayombo alisema akaunti hiyo ilizuiwa kwa siku tatu kabla ya kufunguliwa.

“Ukiona mpaka tumefikia hatua hii ujue suala hilo lilikuwa sugu, hivyo tuliamua kuzuia kwa muda wa siku kama mbili au tatu hivi ili kuhakikisha fedha inapatikana,” alisema.

Kayombo alisema, “Hatukuifungia ila tuliizuia kwani operesheni zake za kuweka ziliendelea kama kawaida, kwa maana ya kuweka fedha isipokuwa walikuwa hawawezi kutoa, lakini sasa tumewafungulia.”

Alisema baada ya siku tatu, mamlaka hiyo ilichukua fedha zote zilizokuwapo na kuiachia akaunti hiyo.

“Katika akaunti tulikuta fedha kiasi lakini pia kwa muda tuliyoizuia kuna nyingine ziliingia, hivyo ilibidi tuchukue zote ili kulipa deni hilo,” alisema.

Hata hivyo, alisema fedha hizo bado hazitoshi kumaliza deni, na kueleza kuwa ni lazima kampuni hiyo ilipe ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Alipoulizwa kiasi cha deni inachodai na kilichosalia, Kayombo alisema hiyo ni siri kati ya mamlaka na mteja wake na anayepaswa kutaja kiasi ni mteja.

“Sheria inatukataza kutaja kiasi tunachodai lakini ninachoweza kusema tu kwa sasa ni kweli tumechukua fedha zote baada ya kuzuia akaunti kwa kushindwa kulipa kodi kwa wakati,” alisema.

Alipoulizwa iwapo mamlaka imetoa muda kwa kampuni hiyo kulipa deni lililobaki, Kayombo alisema, “Sheria ya kodi inataka mtu kulipa kodi yake kwa wakati na si vinginevyo.”

Alisema, “Kama wana sababu ya msingi ya kutaka kuongezwa muda, milango yetu ipo wazi, wafuate taratibu na kuja kuzungumza na kamishna wa kodi.”

Awali, ilielezwa kwamba kwa muda mrefu, StarTimes imekuwa ikisuasua katika ulipaji kodi jambo lililosababisha kuonywa mara kadhaa na TRA.
Loading...

No comments: