Watu 15 wapandishwa Kizimbani kwa kukosa vyoo - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, May 7, 2018

Watu 15 wapandishwa Kizimbani kwa kukosa vyoo


WANANCHI 15 wakazi wa Kijiji cha Gebailumbwa wilayani Longido, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya hiyo wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo la kutokuwa na vyoo na kusababisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Akisoma mashtaka hayo juzi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aziza Temu, Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi wilayani humo, Anzulimu Mihella, alidai kuwa shitaka la kwanza na la pili linawakabili washtakiwa wote kwa pamoja.

Washtakiwa hao ni Oleulei Losinigi (50), Kirusu Taitai (48), Kelepu Kesonyi (35) Lazaro Parteye (38), Joshua Metui (20) Kamete Lemomo (25) Kimare Lamama (38) Lemomo Kokoyo (25) na Zacharia Kabamngasi (33).

Wengine ni Paulo Lemomo (30), Kaika Ngatete (55) Thimotheo Kibangasi (37) na Moko Tataya (75)

Alisema mnamo mwaka 2016 na Aprili 30, mwaka huu, washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa kwa kukaidi amri halali ya kuchimba vyoo, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Afya ya mwaka 2009.

Alisema kosa la pili mnamo mwaka 2016 na Aprili 30, mwaka huu katika nyakati tofauti washtakiwa hao wakiwa wakazi wa kijiji cha Gebailumbwa walikataa kutii amri halali ya Afisa Afya ya kujenga choo ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, kinyume na kifungu cha 111 (1,2) cha Sheria ya Afya ya mwaka 2009.

Kosa la tatu linamhusu mshtakiwa namba mbili, Kirusu Taitai (48) ambapo ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo akiwa mkazi wa Kijiji cha Gibailumbwa, alishawishi wanakijiji kukataa kuchimba choo jambo ambalo ni kosa na ni kinyume kanuni ya adhabu, kifungu cha 390 cha sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Washtakiwa hao waliokuwa wakiongozwa na mwanasheria wao, Nicholaus Senteu, walikana mashtaka na hakimu Aziza, alidai dhamana ipo wazi kwa kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye ni mtumishi wa umma mwenye kusaini bondi ya sh milioni 10 kila mmoja.

Awali wakili, Senteu, aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake yenye masharti nafuu itakayowafanya wakidhi vigezo vya masharti.

Hata hivyo, washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande katika Gereza Kuu la Kisongo jijini Arusha hadi kesi hiyo namba 38/2018 itakapotajwa tena Mei 16, mwaka huu. 
Loading...

No comments: