Bongo Movie wakifanya haya watatisha - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, June 11, 2018

Bongo Movie wakifanya haya watatishaZikiwa zimesalia siku takribani tatu na huku Dunia ikisubiria kwa bashasha kabisa kombe la Dunia nchini Russia, Napenda kuwasilisha barua ya wazi kwa bongo movie kwamba  ulimwengu wa filamu kwa nchi za bara la Amerika na Asia unazidi kukua na  kuwa bora pamoja na kuongezeka thamani.
Nawaza kwa sauti siku moja wasanii wetu kuwaona kwenye majukwaa makubwa kama vile Oscars, Grammy japo ni ndoto ila inawezekana kabisa kufika huko kama watakuwa kutayari.

Huku wasanii wetu wa filamu maarufu kama bongo movie wakitoa kazi zisizo na ushindani katika soko la kimataifa wenzetu bara la Asia wameibuka kwa kishindo sana, wengi watakuwa mashahidi kwa hili hapo awali bara hili lilitawaliwa na filamu za India na China tu lakini sasa kuna Korea na Ufilipino swali la kujiuliza wao wamewezaje? Nini kinaponza sanaa ya filamu Tanzania?
Akili yangu ndogo sana ndipo nikaamua fuatilia sababu kuu ambayo nahisi ndio kikwazo na changamoto kubwa japo zipo zingine ila ni Bajeti na Ushirikiano.


UBORA wa kitu unaanzia kwenye maandalizi yake kuna mambo ya msingi yakifanywa na bongo movie basi sanaa yetu itafika mbali sana.

Bajeti ya Kutosha kumekuwa na kasumba ya kila msanii kuwa na kampuni yake ya uandaaji filamu sipingi la hasha! swali je wanakipato cha kukidhi mahitaji ya soko la sasa ambapo lazima ushindane kwa kutumia teknolojia ya kisasa  ili kupenya katika soko la kimataifa. Wasanii wa Marekani ‘Hollywood’ ndio wanaongoza kwa kazi zao kuwa na bajeti kubwa lakini hatujawahi kusikia kila msanii akiwa na kampuni yake ya uandaaji wa filamu, ndo maana zilizopo zimewekeza kwa kiasi kikubwa na muda mrefu na matokeo yake tunashuhudia kazi zao zikivunja rekodi za mauzo kama vile “BLACK PANTHER”.

Katika suala la bajeti kuna vifaa vingi vya kisasa ambavyo vinatakiwa kununuliwa na kampuni zetu lakini kutokana na ufinyu wa kipato filamu zetu zinakuwa na kiwango cha chini.

Ningependa wajifunze kwa mwanamuziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul Diamond Platnumz alivyoanza kuwekeza kwa gharama kubwa katika video zake za muziki na kuanza kupigwa kwenye vituo vikubwa vya nje, hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa yeye kukamata soko la kimataifa. Leo ukiuliza gharama ya video ya muziki wa Diamond utaambiwq milioni   20 lakini ukiuliza filamu zetu utasikia milioni 9, na tunasubiria kupenya kwenye soko la kimataifa.

Kitu kimoja cha kujifunza sanaa haiwezi inuliwa na mtu mmoja tu, inatakiwa wasanii wote kwa ujumla waungane baadhi waanzishe kampuni ambayo itakuwa inatengeneza filamu wanunue vifaa vingi vya kutosha vya kisasa ili kuendana na kasi ya sasa, waongeze ubunifu katika filamu zao sio unaangalia kitu kimoja tu ‘Plain’.

Ninashukuru na nina imani na waziri mwenye dhamana mheshimiwa Dk Harrison Mwakyembe kwa kuanzisha bodi ya filamu. Bodi hii ikawe mama mlezi kwa wasanii wetu waache kulewa sifa za mtandaoni huku wakiendelea kuteseka na kazi zao kutofika mbali, waje na mikakati ya kuhakikisha wanawasaidia wasanii wetu kimawazo hata kiuchumi kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ili waweze kutoa kazi bora ambazo zitaitangaza vema nchi yangu.


 Naomba kuweka chini kalamu yangu, naamini salamu zangu zitawafikia wahusika na watafanyia kazi machache niliyowaandalia.

Imeandaliwa na Isaya Mwaseba unaweza kutoa ushauri wako kupitia 0752497762 na barua pepe isayamwaseba@gmail.com
Loading...

No comments: