Tanzania Na Zimbabwe Kushirikiana Kibiashara - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, June 29, 2018

Tanzania Na Zimbabwe Kushirikiana Kibiashara


MAENDELEO zaidi yanatarajiwa kupatikana katika nchi za Tanzania na Zimbabwe baada ya marais John Magufuli na mgeni wake, Emmerson Mnangagwa kukubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili.
Tanzania na Zimbabwe zina udugu wa kihistoria ulioasisiwa na mababa wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Robert Mugabe.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa jana ilisema marais hao walifikia makubaliana hayo baada ya mazungumzo rasmi.
Baadaye walizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam katika siku ya kwanza ya ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili ya Rais Mnangagwa, inayomalizika leo.
Taarifa hiyo ilisema: “Mhe. Rais Magufuli amesema mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 18.3, mwaka 2017 ilikuwa Shilingi bilioni 21.1 na kwa ujumla Zimbabwe imewekeza nchini Tanzania kiasi cha Shilingi bilioni 72.2, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano wa mataifa hayo.
“Kufuatia hali hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema wamekubaliana tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission-JPC) ambayo mara ya mwisho ilikutana mwaka 1998, ikutane baada ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu, ili kujadili vikwazo na kutafuta majawabu ya kukuza biashara na uwekezaji baina ya mataifa haya mawili.

“Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Mnangagwa kwa kukubali mwaliko wa kuja kutembelea hapa nchini Tanzania ikiwa ni miezi 6 tangu aingie madarakani na akiwa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu na amempongeza kwa namna anavyochukua hatua mbalimbali ikiwamo kuimarisha demokrasia, kukuza uchumi na kumpa heshima Baba wa Taifa la Zimbabwe, Rais mstaafu Robert Mugabe”.
Taarifa pia ilimkariri Rais Magufuli akisema, “Nakupongeza kwa namna unavyofanya juhudi za kusukuma mbele maendeleo ya Zimbabwe, na pia nakupongeza kwa jinsi mnavyomthamini Mzee Robert Mugabe na kumpa heshima ya kuwa Baba wa Taifa la Zimbabwe, yeye na viongozi wenzake Julius Nyerere wa Tanzania, Keneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa DRC, Samora Machel wa Msumbiji na wengine wametoa mchango mkubwa katika juhudi za ukombozi wa Bara la Afrika, tuna kila sababu ya kuwaenzi na kuwatunza” amesema Mhe. Rais Magufuli.”
Kwa upande wake, Rais Mnangagwa alimshukuru Rais Magufuli kwa kumwalika na kusisitiza kuwa Zimbabwe inatambua mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Taifa hilo pamoja na mataifa mengine ya Afrika ambayo yaliendesha harakati zao za ukombozi nchini, taarifa ilisema zaidi.
Amos Nyanduku
Loading...

No comments: