Mahakama yatengua hukumu kesi ya ufukwe wa Oysterbay - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, July 16, 2018

Mahakama yatengua hukumu kesi ya ufukwe wa Oysterbay

Mahakama ya Rufani imetengua hukumu na mwenendo wa kesi ya mkataba wa uendelezaji wa ufukwe wa Oysterbay kwa kuwa Jaji Aghaton Nchimbi aliyetoa hukumu hiyo hakueleza sababu za kuisikiliza yeye, badala ya jaji wa awali.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo imeirudisha kesi hiyo Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ili ianze kusikilizwa upya na jaji mwingine tofauti na aliyetoa hukumu hiyo.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoongozwa na Kipenka Mussa akishirikiana na Jaji Richard Mziray na Jaji Gerald Ndika.

Jopo hilo la majaji lilisikiliza rufaa ya kesi ya Manispaa ya Kinondoni dhidi ya Kampuni ya Q Consult Limited.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Nchimbi Julai 23, 2015, ilikubaliana na madai ya mlalamikaji, Q Consult Limited kuwa Manispaa ya Kinondoni ilivunja makubaliano ya uendelezaji wa ufukwe huo kwa kutotekeleza majukumu yake.

Hivyo, Jaji Nchimbi aliiamuru manispaa kutekeleza wajibu wake kulingana na makubaliano ya mkataba huo na pia akaiamuru imlipe mdai fidia ya Sh500 milioni.

Manispaa ya Kinondoni ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo, ikidai kuwa Jaji Nchimbi aliyetoa hukumu hiyo hakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyoandikwa na Jaji Ndika kwa niaba ya jopo hilo, ilieleza kuwa Jaji Nchimbi kutokueleza sababu za kuisikiliza kesi hiyo kunamfanya akose mamlaka ya kushughulika nayo.

Katika hukumu hiyo ambayo Gazeti la Mwananchi imeiona nakala yake, Mahakama ya Rufani imeeleza msimamo wa kisheria kwamba jaji au hakimu anapolazimika kuendesha kesi ambayo tayari ilishaanza kusikilizwa na jaji/hakimu mwingine ni lazima aeleze sababu za yeye kuisikiliza.

Huku ikirejea hukumu za kesi mbalimbali pamoja na kifungu cha 214 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Mahakama ya Rufani imesema kutokuwepo kwa sababu yoyote kwenye kumbukumbu za shauri husika kunamfanya jaji/hakimu huyo asiwe na mamlaka kuiendesha.

Imesisitiza kuwa matokeo yake mwenendo wote wa shauri hilo ambao umeshaendeshwa na jaji/hakimu mwingine unakuwa ni batili.
Loading...

No comments: