MAONI YA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2018/2019 - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, July 5, 2018

MAONI YA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2018/2019

Dar es Salaam, 04.07.2018 | Muungano wa Asasi za Kiraia zinazofanya kazi na kufuatilia masuala ya sekta ya kilimo na bajeti Tanzania tunatoa maoni ya pamoja kuhusu bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 iliyoidhinishwa hivi karibuni.Serikali imetenga kiasi cha TZS 32.47 trilioni kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ikijumuisha kiasi cha TZS 20.46 trilioni kwa matumizi ya kawaida (sawa na asilimia 63) na kiasi cha TZS 12 trilioni kwa matumizi ya miradi ya maendeleo (sawa na asilimia 37). Serikali imetenga jumla ya kiasi cha TZS 170.27 bilioni kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo ni sawa na asilimia 0.52 tu ya bajeti ya Serikali.Utengaji na utoaji huu mdogo wa fedha za bajeti katika Wizara ya kilimo umeendelea kuleta changamoto nyingi ikiwemo kutoanza na kutoendelea kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo; kutopatikana kwa mbegu, mbolea na pembejeo nyingine muhimu kwa kutosheleza na kwa muda sahihi kwa wakulima (hususani wakulima wadogo wadogo); uhaba wa maafisa ugani na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha; kuharibika kwa mazao baada ya mavuno; tafiti hafifu; na kuendelea kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.Hivyo, muungano huu wa asasi za kiraia tunapendeleza yafuatayo:1. Serikali na Wizara ya Kilimo kuboresha jitihada za Ukusanyaji wa Mapato kwa Vyanzo vya Ndani: ili kuweza kuongeza bajeti na utoaji wa fedha za utekelezaji kama zilivyoidhinishwa. Wizara inaweza kutumia fursa mbalimbali ikiwemo kutafuta ithibati (accreditation) au kushirikiana na taasisi nchini ambazo zimepata ithibati kuomba fedha katika mifuko ya fedha za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ‘Green Climate Fund (GCF)’ na ‘Adaptation Fund (AF)’. Pia, kuboresha uwekezaji na upatikanaji wa masoko ili kuongeza uzalishaji, mauzo ya malighafi na bidhaa, na matumizi ya miundombinu bora ya kilimo. Vilevile, kiasi cha mapato yanayopatikana kutokana na sekta ya kilimo kiwekezwe katika sekta hiyo ikiwemo mapato ya mauzo ya nje ya zao la korosho ambayo kwa sasa yanaenda ofisi ya hazina.Serikali pia iongeze jitihada na kuweka mikakati mahususi na kabambe ya uibuaji wa vyanzo vipya na ukusanyaji zaidi wa mapato. Japokuwa kumekuwa na jitihada za kuimarisha usimamizi na utoaji elimu kwa walipa kodi bado kumekuwepo na changamoto katika mfumo wa ukusanyaji. Serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) iboreshe mfumo huo kwa kuweka makadirio halisia na kuondoa ushurutishwaji wa nguvu kubwa kwa walipa kodi. Hii itasaidia biashara nyingi kutofungwa na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yatawekezwa katika sekta muhimu ikiwemo kilimo.2. Kuboresha Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo hususani kwa Wakulima wadogo wadogo na Wanawake: ikiwa ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa, Serikali inahitajika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ikiwemo – kuongeza uwekezaji kwa wakulima wadogo wadogo na kuweka kipaumbele katika maeneo ya umwagiliaji wenye ufanisi; upatikanaji wa pembejeo na kwa wakati; na ufanisi wa huduma za ugani. Pia, kuboresha mfumo wa huduma za kifedha na masoko hususani katika maeneo ya vijijini ambayo wakulima wadogo wadogo wanafanya uzalishaji. Mfumo wa kupitia katika vyama vya ushirika kwa masoko ni mzuri japokuwa unahitaji kuboreshwa zaidi kwa kuwapa wakulima wadogo wadogo uhuru wa kuchangua mfumo mzuri wa masoko.Kwa kuwa wakulima wanawake ni wazalishaji wakuu na wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa sekta ya kilimo; Serikali na Wizara husika ya kilimo inahitajika kutambua mchango huo kwa kuboresha uwekezaji ili waweze kupata huduma muhimu ikiwemo ugani, mikopo, bima na masoko. Pia, kuwezesha kushiriki kikamilifu katika mipango na utekelezaji wa sera, mikakati, miradi na bajeti. Vilevile, masuala ya jinsia yahuishwe kikamilifu katika sera, mikakati, miradi na bajeti hizo.3. Kuchochea mchakato wa kujumuisha masuala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika bajeti: kwa kuweka ‘Kifungu cha Bajeti au Kasma’ mahususi ya mabadiliko ya tabianchi katika bajeti ya Wizara (ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango). Pia, kuboresha uelewa wa maafisa katika idara zote za Wizara kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na namna ya kujumuisha masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika bajeti za idara zao na Wizara kiujumla.4. Wizara iboreshe mfumo wa upatikanaji wa taarifa za bajeti na zenye uwiano. Wizara iimarishe uratibu ikishirikiana na Wizara ya Fedha na Wizara na taasisi nyingine zinazohusika na uandaaji na uhifadhi wa taarifa. Pia, kuboresha uhifadhi wa taarifa katika mfumo wa mtandao ambao utakuwa rahisi kupatikana na kueleweka.


Loading...

No comments: