Profesa Mbarawa alivyotinga DAWASCO Baada ya Kukabidhiwa Wizara Ya Maji


Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) imejipanga kuwasajili wamiliki wa visima binafsi jijini hapa ili kuwatambua na kutibu maji yao ili wasipate magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama.

Akizungumza leo Julai 4 wakati akimpokea Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha  wananchi wanapata maji safi na salama.

Luhemeja amesema wenye visima binafsi wanaouza maji watakuwa wanaangaliwa kwa karibu ili kukaguliwa maji wanayouza ili wasisababishe madhara kwa watumiaji wa bidhaa hiyo muhimu.

“Mwaka ujao, tutawasajili wote wenye visima na, tutawapa leseni na tutakuwa tunayatibu maji yao na wale wanaouza maji yao tutakuwa tunawasimamia,” amesema mkurugenzi huyo wakati akieleza mipango ya taasisi yake kwa Waziri Mbarawa.

Mtendaji huyo amesema wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo wamesaini makubaliano ya utendaji (performance agreement) ambayo yanaonyesha majukumu yao ambayo yanatarajiwa kufikiwa kwa mwaka.

Kwa upande wake, Profesa Mbarawa amewataka wataalamu wa Dawasco kwenda mitaani kudhibiti upotevu wa maji yanayovuja. Amesema wakifanya hivyo watapata faida kwenye huduma wanayoitoa kwa wananchi.

Amesisitiza kwamba jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha ili kufikia lengo la asilimia 95 ambalo limewekwa bayana kwenye Ilani ya Chama cha mapinduzi (CCM).

“Hakuna sababu ya msingi ya kuwafanya Watanzania wakose maji. Sote tujipange na tuhakikishe tuawapatia maji wananchi, wako wateja wengi huko mitaani wanahitaji maji lakini hawajafikiwa,” amesema Profesa Mbarawa wakati akizungumza na wafanyakazi wa Dawasco alipokwenda kujitambulisha baada ya kurudishwa wizara ya maji na umwagiliaji.

Post a Comment

0 Comments