Bwege ataka akamatwe yeye badala ya Zitto - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, August 3, 2018

Bwege ataka akamatwe yeye badala ya Zitto


Mbunge wa Kilwa kusini –CUF Suleiman Bungara maarufu Bwege ameingilia ugomvi wa Zitto Kabwe na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kwa kumtaka Waziri huyo amkamate yeye kwanza kwa kuwa yeye ndiye alimuita Zitto kwenye mkutano wake.

Kauli hiyo ya Bwege imekuja baada ya waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola kumtaka mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe kujisalimisha polisi mwenyewe kwa  kosa la kutoa  kauli za kichochezi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Kilwa kusini mkoani Lindi.
" Mh Zitto mimi ndiye niliyemwandikia barua aje kwenye mkutano wangu, naona ni kukandamiza haki na uhuru wa wabunge siyo sahihi kumkamata Zitto Kabwe kwa sababu mimi ndiye niliyemuita kama kunikamata wanikamate mimi".

Amemtaka waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola kujali na kufuata sheria za nchi katika utendaji kazi wake kwa kuwa Tanzania ni nchi ya demokrasia inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na siyo kwa amri.

Bwege amesema Waziri Lugola ni mbunge aliyepata uwaziri, hivyo anamshauri kabla hajasema jambo lolote hadharani ni vema akawatumia wanasheria waliopo kwenye wizara yake kwa ajili ya kumshauri mambo muhimu ya kuongea hadharani badala ya  kuongea mambo ambayo kisheria hayapo.

Mbunge huyu ameongeza kuwa kwa upande wake amepigiwa simu na polisi mkoani Lindi wakimtaka kuripoti kituoni hapo na baada ya kufanya hivyo kutoka na maelezo yake amefunguliwa jalada la uchunguzi katika kesi ya uchochezi.

Aidha baada ya agizo la Waziri Kangi Lugola la kutaka Zitto Kabwe aripoti kituo cha polisi mkoani Lindi ndani ya siku mbili vinginevyo akamatwe popote alipo, jeshi la polisi kupitia kwa msemaji wake Barnabas Mwakalukwa lilitoa taarifa kuwa polisi wamefungua jalada la  uchunguzi dhidi ya kauli zilizotolewa na Mbunge Zitto Kabwe ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo.

Hata hivyo kupitia kwa  Katibu Kamati ya Uenezi na Mawasiliano  Ado Shaibu chama cha ACT Wazalendo kilitoa tamko rasmi kwamba baada ya kushauriana na wanasheria wa chama wamekubaliana kwamba kiongozi wao Zitto Kabwe hatakwenda kuripoti polisi kama waziri Lugola alivyoagiza kwa kuwa waziri huyo hana mamlaka kisheria ya kutoa agizo hilo na kwamba wenye mamlaka ni polisi.

Hata hivyo , hadi sasa Zitto hajaripoti kituo chochote cha polisi kama alivyotakiwa na waziri Lugola, kwa sasa anaendelea na mikutano yake ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Buyungu kama kawaida.
Loading...

No comments: