Tigo Pesa yatoa Riba ya TSH 2.35 Billion kwa Wateja - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, August 23, 2018

Tigo Pesa yatoa Riba ya TSH 2.35 Billion kwa Wateja


Yatoa Riba  ya Robo ya pili ya Mwaka Kutoka Kwenye Akaunti Za Wateja wa Tigo Pesa.

Dar es Salaam, 23 Agosti 2018: Wateja wa mtandao unaongoza kwa maisha ya kidigitali nchini, Tigo Tanzania ambao wamejisajili  na huduma ya kifedha ya Tigo pesa wamepokea TSH 2.35 billioni kama gawio la riba ya robo ya mwaka kutoka kwa akaunti za wateja wa Tigo Pesa.
Akitangaza gawio hilo la riba ya robo ya pili ya mwaka jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari alisema, “Gawio hili ni uthibitisho zaidi kuwa Tigo Pesa ni Zaidi ya Pesa. Kila robo ya mwaka tunatoa gawio la riba kwa wateja wetu kwa kuzingatia kiwango cha fedha kilichopo katika akaunti ya Tigo Pesa ya mteja husika.

Tigo inajivunia mtandao unaokua kwa kasi zaidi nchini wa wateja waliosajiliwa 12 milioni, zaidi ya watumiaji milioni 7 wa huduma yake ya kifedha ya Tigo Pesa, pamoja na mtandao mpana wa wafanyabiashara zaidi ya 40,000 na mawakala 85,000 waliosambaa kote nchini.

Tigo ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani kutoa gawio la riba itokanayo na akaunti yake maalum ya huduma za kifedha. Kuanzia mwaka 2014, kampuni hiyo imetoa gawio la jumla ya TSH 81.8 billioni kwa wateja wake wanaopokea malipo kwa kuzingatia thamani waliyo nayo katika akaunti zao za Tigo Pesa kwa kuzingatia kanuni za Benki Kuu,’ Simon alisema.  

Alibainisha kuwa ongezeko kubwa la wateja ambao wanaotumia huduma za kifedha kwa njia simu limetokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Tigo katika kupanua huduma zake, kufanya ubunifu unaozingatia matakwa ya wateja, teknologia ya kisasa ya pamoja na utoaji wa huduma za mahususi zinazoongeza thamani kwa wateja wake.

Tigo Pesa imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania za kupanua wigo wa upatikaji wa huduma za kifedha nchini. Tigo pia inafungua ukurasa mpya wa uchumi na maisha yasiyotegemea pesa taslim kwa kupanua na kuboresha huduma zake na kubuni njia mpya na bora zaidi za wateja wake kufurahia huduma za haraka, salama, uhakika, za fedha kwa njia ya simu za mkononi popote walipo.

Ili kuwapa wateja wake uwezo zaidi juu ya miamala yao, Tigo ndio kampuni ya kwanza ya simu nchini kuanzisha huduma ya Jihudumie inayowezesha wateja kuzuia kwa haraka miamala iliyokosewa ya kutuma fedha kwa wateja wengine wa Tigo, bila kuhitaji msaada wa moja kwa moja wa kitengo cha huduma kwa wateja.

Pia, Tigo ndio mtandao wa kwanza nchini kuleta huduma ya Masterpass QR inayowezesha wateja kulipia huduma na bidhaa kwa urahisi na usalama kwa kuscani nembo ya Masterpass Quick Response (QR) inayopatikana katika maelfu ya maduka nchini.

Tigo Pesa imeunganishwa na mfumo wa Serikali wa malipo ya mtandao (GePG) kupitia namba za USSD, App ya Tigo Pesa na kwa kuscan nembo ya QR, ili kuwezesha wateja kufanya malipo ya haraka kwa mashirika ya kiserikali zaidi ya 150 nchini.

Katika kupanua wigo wa mfumo wake wa malipo, Tigo imeingia katika makubaliano ya kimkakati na kampuni ya kiteknologia ya Uber ili kuwezesha wateja wake kutumia app ya  Uber bure pasipo gharama za intaneti. Vile vile, kila wanapofanya miamala ya Tigo Pesa, wateja wa Tigo Pesa wanafurahia huduma za usafiri wa Uber kwa punguzo la bei.

Kwa kipindi cha miaka mingi sasa, Tigo imeongoza katika mageuzi ya soko la huduma za mawasliano. Mwaka 2014, Tigo ilikuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano Africa kuzindua huduma ya kifedha iliyoruhusu wateja wa mitandao tofauti kufanya miamala baina ya mitandao yao. Mwaka huo huo, Tigo ilizindua huduma ya kwanza ya kifedha Afrika Mashariki iliyowezesha utumaji wa fedha kutoka nchi moja hadi nyingine kwa kuzingatia thamani ya sarafu ya nchi husika, hivyo kurahisisha na kuongeza uhamishaji wa fedha kuvuka mipaka ya nchi.
Mifano hii inathibitisha kuwa Tigo inazidi kufanya ubunifu unaozingatia mahitaji maalum ya wateja na kutoa huduma bora na rahisi zaidi zinazoboresha maisha nchini kote.

Loading...

No comments: