Wakili Kesi Ya Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Ajitoa - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, August 23, 2018

Wakili Kesi Ya Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Ajitoa

Wakili Jeremiah Mtobesya, anayewatetea viongozi tisa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, amejitoa katika kesi hiyo baada ya mahakama kukubaliana na upande wa jamhuri kwamba washtakiwa wasomewe maelezo ya awali leo wakati leo kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Amedai akiendelea kuwatetea washtakiwa hao, haki haitatendeka.

Wakili huyo alijitoa kuwatetea washtakiwa hao mara baada ya Mahakama ya Hakimu Kisutu kuyatupilia mbali maombi yao ya kutaka kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka huu iahirishwe katika Mahakama ya Kisutu ili kusubiri   maombi yao na rufaa yaliyopo Mahakama ya Rufani yasikilizwe na kutolewa maamuzi.

Hata hivyo Hakimu Mashauri aliyatupilia mbali maombi hayo kwa sababu kifungu cha sheria walichotumia cha 225 (1) (2) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho2002 hakiipi mamlaka hayo.

Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa uamuzi wa Mtobesya ambapo baada ya kujitoa alibeba kila kilicho chake mezani na kutoka nje ya chumba cha mahakama.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika.

No comments: