Bilioni 216 Zatumika Kukamilisha Miradi ya Umeme Kanda ya Kusini - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, September 15, 2018

Bilioni 216 Zatumika Kukamilisha Miradi ya Umeme Kanda ya Kusini


Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Serikali  imetumia kiasi cha shilingi bilioni 216 kukamilisha mradi wa Umeme  wa Makambako hadi Songea ikiwa ni moja ya miradi ya kimkakati yenye lengo ya kufanikisha sera ya Tanzania ya viwanda.

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Septemba mitambo ya mradi huo itawashwa na wananchi wa mikoa ya Njombe na Ruvuma wataanza kufurahia umeme wa uhakika kutoka gridi ya taifa.

“Mradi  huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani wataunganishiwa umeme kwa  bei nafuu ya mradi wa REA  ambayo ni  elfu 27 tu  na kuwanufaisha wateja  22,700 hali itakayowawezesha wananchi  kutumia umeme huo kwa ujenzi wa viwanda na shughuli za maendeleo katika maeneo yao” Alisisitiza Dkt. Kalemani

Akifafanua zaidi Dkt. Kalemani  amesema kuwa  kukamilika kwa mradi huo kutaokoa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 9.1 ambazo zinatumika kununua mafuta mazito yanayotumika kwenye mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Madaba, Ludewa, Mbinga, Namtumbo na Songea Mjini.

Akielezea ujenzi wa mradi huo uliotekelezwa na Serikali ya Tanznaia kwa kuhsirikiana na Serikali ya Sweden, Waziri Kalemani amesema mradi huo umetekelezwa kwa awamu mbili. “Sehemu  ya kwanza ya mradi huu imehusisha  ujenzi wa vituo vitatu vya kupooza na kusambaza umeme mkubwa wa msongo wa KV 220 vilivyojengwa Makambako, Madaba na Songea na sehemu ya pili ilihusisha ujenzi wa miundo mbinu ya kusafirisha umeme”.
Loading...

No comments: