Mwenyekiti
Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd. Dk. Reginald Mengi (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika hafla fupi
iliyofanyika ofisi za IPP ya kutambulishwa rasmi na TFF kuwa mlezi wa
timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’
jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Bw. Wallace Karia.
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Wallace Karia
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa
kumtambulisha rasmi Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd. Dk.
Reginald Mengi (kulia) kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri
chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ katika hafla fupi iliyofanyika
katika ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.
Mwandishi
wa Habari za Michezo Clouds TV, Jacob Mbuya (wa pili kushoto) akiuliza
swali kwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17,
‘Serengeti Boys’ Dk. Reginald Mengi (hayupo pichani) kuhusiana na
malezi ya vijana hao ndani ya kambi na nje ya kambi wakati wa hafla fupi
ya TFF kumtangaza rasmi kwa vyombo vya habari kuwa mlezi wa timu hiyo
iliyofanyika katika ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MLEZI
wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti
Boys’, Dk. Reginald Mengi, amesema kuwa kikosi hicho kina kila sababu ya
kufanya kweli katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
zinazotarajiwa kufanyika hapa nchini Aprili mwakani.
Mengi
aliyasema hayo jana baada ya kutambulishwa rasmi na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kuwa mlezi wa timu hiyo, hafla iliyofanyika jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa TFF, Walace Karia, makamu wake,
Athuman Nyamlani na Katibu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau.
Mwenyekiti
huyo wa Makampuni ya IPP, alisema kuwa amefurahi mno kupewa nafasi hiyo
ya kuwa mlezi wa Serengeti Boys, ukizingatia ni miongoni mwa wadau wa
soka la vijana, akiwa ameifuatilia mno timu hiyo kwa muda mrefu.
“Hakuna
sababu ya Serengeti Boys kutokuwa washindi, tunaamini tunaweza na timu
hii itailetea Tanzania heshima kubwa. Shakira (mwanamuziki wa Colombia)
aliimba ‘This time is for Africa’ wakati wa Kombe la Dunia 2010, na sisi
tunasema ‘This time is for Tanzania (safari hii ni zamu ya Tanzania).
“Tuna
kila kitu cha kutufanya tuwe washindi, wanachotakiwa vijana kufanya ni
kujiamini. Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha timu inapata maandalizi
ya kutosha ili iweze kufanya vizuri,” alisema.
Alimtaka kila Mtanzania kujivunia timu hiyo ya Serengeti Boys huku akiahidi kutowaangusha watanzania kutokana nafasi hiyo.
“Nawahakikishia Serengeti Boys itashinda mechi zote na kutwaa ubingwa,” alisisitiza Dk. Mengi.
Kwa
upande wake, Karia alisema: “TFF tunafarijika kwa ndugu Mengi kukubali
kuwa mlezi wa timu hii ya Serengeti Boys na tunaamini kwa pamoja
tutaifanya timu hii kuwa msingi mzuri katika maendeleo ya ustawi wa soka
la vijana.”
Alisema
kuwa mkakati wao ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vema katika michuano
hiyo ikiwa kama mwenyeji, lakini pia kukinukisha kwenye fainali za
Kombe la Dunia nchini Peru Oktoba mwakani na hata zile za mwaka 2026
nchini Mexico na Peru.
“Tunawaomba
wadau wa soka nchini na viongozi mbalimbali kumuunga mkono Dk. Mengi
katika majukumu yake hayo kwani itakuwa ni fedheha kwa Taifa kama
wenyeji wa michuano iwapo ubingwa utatoka nje ya Tanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment