Meneja wa Wakala
wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo (kushoto),
akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack
Kamwelwe (kulia), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa
pamoja kilichopo wilayani Manyoni, mkoani Singida.
NA WUUM, SINGIDA
SERIKALI imesema imeshaanza kutoa misamaha ya kodi kwa
mikataba ya ujenzi na matengenezo ya
miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na madaraja ambayo
ilitakiwa kusamehewa kulipa kodi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi
hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akikagua hatua za
ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (One Stop Inspection Station), wilayani
Manyoni mkoani Singida, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Isack Kamwelwe amesema kuwa mradi huo umechelewa kukamilika kutokana na
mkandarasi kutopata msamaha wa kodi kama jinsi ilivyopangwa na hivyo kuathiri
mtiririko wa fedha katika utekelezaji wa wake.
"Serikali imeanza kutekeleza misamaha ya kodi
iliyokwama katika miradi inayoendelea na inayotarajiwa kuanza hapa nchini
ikiwemo huu mradi na mingine mingi", amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.
Mhandisi Kamwelwe amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Impresa
di Construction Ing E. Mantovani S. p. A con socio unico Via Belgio anayejenga
kituo hicho kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya muda aliyoomba
kuongezewa kwani hataongezewa muda mwingine.
"Nahitaji kituo hichi kikamilike ifikapo mwezi Februari mwakani, kwani haya ni maazimio ya pamoja ya nchi za wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kupunguza ucheleweshwaji wa usafirishaji wa
mizigo kupitia barabara ya kati kuelekea nchi jirani", amesisitiza
Mhandisi Kamwelwe.
Aidha, Waziri Kamwelwe ameeleza kuwa ukamilikaji wa vituo
hivyo utapunguza muda na gharama za usafirishaji wa mizigo kupitia barabara ya
Ukanda wa Kati (Central Corridor) kwani hadi sasa magari makubwa yanasimama
vituo 31 kutokea Dar es Salaam hadi mipaka ya Burundi, Rwanda na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Awali akitoa taarifa ya mradi kwa Waziri huyo, Meneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo
ameeleza kuwa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha Manyoni umefikia asilimia
60 na ujenzi huo unaenda sambamba na ujenzi wa kituo kilichopo Nyakanazi mkoani
Kagera.
Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho utahusisha uwekaji wa
mizani ya mwendo, ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA), Polisi, Uhamiaji, kituo cha
mapumziko na mafunzo kwa wasafirishaji, maegesho ya magari makubwa na nyumba za
watumishi.
Mradi wa ujenzi wa vituo vikuu vya ukaguzi wa pamoja wa
magari makubwa yanayoenda nje ya nchi unahusisha vituo vitatu ambavyo ni
Vigwaza, Manyoni na Nyakanazi kwa umbali
wa takribani kilomita 500 kutoka kituo kimoja hadi kingine ikiwa na lengo la
kuondoa msongamano wa magari makubwa kwenye vituo vilivyopo.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia),
akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida
Mhandisi Leonard Kapongo (wa pili kushoto), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi
wa kituo cha ukaguzi wa pamoja katika kijiji cha Muhalala, wilayani Manyoni,
mkoani humo.(PICHA NA WUUM)
No comments:
Post a Comment