SERIKALI YAFUTA BAADHI YA TOZO NA ADA ZILIZOKUWA ZIKITOZWA NA OSHA KUVUTIA UWEKEZAJI - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, September 20, 2018

SERIKALI YAFUTA BAADHI YA TOZO NA ADA ZILIZOKUWA ZIKITOZWA NA OSHA KUVUTIA UWEKEZAJI


  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika katika kujenga uchumi wa viwanda ikiwemo kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa zikitozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) ikiwemo ada ya Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi hii leo Jijini Dodoma Septemba 20, 2018.

NA BEATRICE LYIMO-MAELEZO DODOMA.

SERIKALI imefuta baadhi ya ada na tozo zisizoondoa wajibu wa muajiri kulinda Afya za Wafanyakazi  ili  kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Hayo yamesemwa leo, Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa katika Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) ili kuchangia katika kutekeleza azma ya Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.

Waziri Mhagama amebainisha kuwa lengo la kufuta  tozo na ada hizo ni Kuboresha mazingira ya biashara, kupunguza gharama za uendeshaji kwa wawekezaji na waajiri.

"Tumefuta ada mbalimbali ikiwemo ada ya fomu ya usajili ambayo ilikuwa  shilingi 2000 kwa lengo la kupunguza gharama, tumefuta ada ya usajili wa maeneo ya kazi kwa kuzingatia ukubwa wa eneo ambayo ilikuwa ikitozwa kwa kiasi cha shilingi 50,000 hadi 1,800,000 kulingana na eneo hivyo usajili kwa sasa ni bure" ameeleza Waziri Mhagama.

Aidha,  amesema kuwa, Serikali imefuta ada ya Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi iliyokuwa ikitozwa Tshs 200,000 kwa mwaka kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara hivyo kwa sasa leseni hiyo itatolewa bure.

Pia, Tozo ya siku ya Ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya kwa kuzingatia idadi ya wafanyakazi ya shilingi  450,000 imefutwa kwa lengo la kupunguza gharama ili kutoa elimu kwa wahitaji wengi zaidi.

Hata hivyo, Waziri Mhagama amesema kuwa OSHA imejikita katika utoaji Elimu kwa wadau kuhusu takwa la kisheria la kulinda afya za wafanyakazi nchini mahala pa kazi katika Kanda mbalimbali na kusimamia mifumo ya utendaji wa watumishi wa OSHA ili kuondoa mianya ya rushwa na kukuza uzalendo na uwajibikaji.

 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) Bi. Hadija Mwenda akizungumzia umuhimu wa kulinda afya na Usalama  kwa wafanyakazi katika maeneo ya kazi wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) na waandishi wa habari  leo Jijini Dodoma.

  Mkuu wa Kitengo Cha Sheria kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) Bi. Joyce Mwambungu akifafanua kwa waandishi wa habari juu ya baadhi ya Tozo za kikanuni ambazo zimefutwa kwa mujibu wa Sheria. (Kushoto) ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) Bi. Hadija Mwenda na Mkurugenzi wa Usalama na Afya (OSHA) Bw. Alex Ngata.


Baadhi ya waandishi wa habari na maofisa wa OSHA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokutana nao hii leo kuzungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali katika katika kujenga uchumi wa viwanda ikiwemo kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa zikitozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) leo Jijini Dodoma.
Loading...

No comments: