KATIBU MKUU WA CCM DKT. BASHIRU ALLY KATIKA ZIARA YA KIMKAKATI NCHINI CHINA - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Sunday, October 14, 2018

KATIBU MKUU WA CCM DKT. BASHIRU ALLY KATIKA ZIARA YA KIMKAKATI NCHINI CHINA

  NA K-VIS BLOG.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kamaradi Dkt. Bashiru Ally (pichani juu) ameondoka nchini Oktoba 14, 2018 na baadhi ya viongozi wa chama hicho kuelekea nchini China kwa ziara ya kimkakati inayolenga kuongeza mahusiano kati ya CCM na Chama Cha Kikomunisti cha Watu wa China (CPC), taarifa ya Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa na Idara ya Itikadi na Uenezi ya chama hicho imesema.
Akizungumza kabla ya kuanza safari hiyo, Kamaradi Bashiru ameelezea safari hiyo kwamba ni ya kimkakati na inalenga kuimarisha mahusiano kati ya CCM na CPC. Aidha amesisitiza safari hiyo pamoja na mambo mengine ujumbe wa viongozi hao utakwenda kubadilisha uelewa, uzoefu na kujifunza mikakati ya kujitegemea kirasilimali ili kuendesha Chama, namna bora na bunifu ya kuendesha Miji na Majiji nchini na namna bora ya kujenga mahusiano kati ya Chama na Serikali katika kutoa maendeleo kwa watu.
Ujumbe wa Chama Cha Mapinduzi umejumuisha kwa uwakilishi viongozi wa Chama Taifa ikiwamo wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Jumuia za Chama, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Wajumbe wa Bodi za Kampuni za Chama na Maafisa wa Chama kutoka Ofisi Ndogo ya Makao Makuu. Chama Cha Mapinduzi katika ujumbe huu kimejumuisha maafisa wawili wa Serikali ili nao wakajifunze kama sehemu ya ujumbe huo.
Ujumbe wa CCM utakuwa Nchini China kwa siku 10 na utakuwa na fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali wakiangazia fursa za mashirikiano na uwekezaji kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Taifa.
Wakati huo huo Kamaradi Bashiru ametumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa dhati watanzania wakaazi wa Wilaya ya Liwale na Jimbo la Liwale kwa uchaguzi mzuri uliokamilika kwa Amani na usalama na kukiwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupiga kura ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea wake Zuberi Kuchauka kimeibuka na ushindi wa kishindo.
Huu ni muendelezo wa mikakati ya kukuza mahusiano ya kimataifa, diplomasia ya siasa na uchumi kwa manufaa ya nchi yetu Tanzania.

Loading...

No comments: