NEC YATANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI JIMBO LA BABATI MJINI NA UKEREWE - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, October 19, 2018

NEC YATANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI JIMBO LA BABATI MJINI NA UKEREWE


Na Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata 26 za Tanzania Bara.

Majimbo hayo ni pamoja na Jimbo la Babati Mjini lililopo Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara na Jimbo la Ukerewe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza

Akisoma taarifa kwa umma Jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi) Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk amesema kwamba uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro na Serengeti pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.

“Nafasi hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa Majimbo hayo Bwana. Joseph Michael Mkundi (Ukerewe) na Bi. Pauline Philipo Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” alisema Jaji Mbarouk.

Alifafanua kwamba Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Majimbo hayo mawili.

“Uchaguzi huu mdogo katika Majimbo ya Babati Mjini na Ukerewe utafanyika sambamba na uchaguzi katika Majimbo ya Serengeti, Simanjiro pamoja na Kata 21 zilizotangazwa awali….,” alisema.

Akisoma ratiba ya uchaguzi huo, Jaji Mbarouk amesema “fomu za uteuzi  wa  wagombea zitatolewa kati ya  tarehe 28 Oktoba hadi 3 Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 4 Novemba  hadi tarehe 1 Desemba mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu”.
Loading...

No comments: