Nyoni awaangukia Watanzania - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Wednesday, November 21, 2018

Nyoni awaangukia Watanzania


BEKI wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Erasto Nyoni, amewaambia Watanzania kuwa, bado hawajamaliza kazi, hivyo waendelee kuwasapoti.
Nyoni ametoa kauli hiyo baada ya wikiendi iliyopita timu hiyo kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Lesotho ukiwa ni mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).
Katika mchezo huo wa Kundi L uliochezwa kwenye Uwanja wa Setsoto uliopo Maseru, Lesotho, Taifa Stars ilitakiwa ishinde ili ifuzu moja kwa moja, lakini haikuwa hivyo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nyoni ambaye kwenye mchezo huo alikuwa nahodha, alisema: “Watu wasichukulie kama vile ndiyo kazi imeisha, hapana, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu Afcon.
“Tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono, tunajua matokeo haya hayakuwa mazuri, lakini tunawataka watupe sapoti tuweze kufanya vizuri dhidi ya Uganda.”
Ikumbukwe kuwa, Taifa Stars ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo ikiwa na pointi tano sawa na Lesotho, inatakiwa kushinda mechi ya mwisho dhidi ya Uganda, huku ikiomba Lesotho ipoteze mbele ya Cape Verde au kutoka sare ili ifuzu Afcon.

KWA HISANI YA GLOBAL PUBLISHERS

Loading...

No comments: