Tanzania yaandaa kongamano la uchumi na siasa Dar es Salaam

Kongamano maalumu linaloangalia hali ya uchumi na siasa nchini Tanzania limeandaliwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Tanzania imeandaa kongamano maalumu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linaloangalia hali ya uchumi na siasa nchini humo. Kkwa mara ya kwanza kongamano hilo limehudhuria na Rais John Magufuli ambaye wiki ijayo atatimiza miaka mitatu tangu aingie madarakani.
Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi Nkrumah limewaleta pamoja maprofesa kutoka chuoni hapo, wanasiasa, viongozi walioko serikalini na linatoa fursa kwa washiriki kuchambua hali ya uchumi wa taifa na mwelekeo wa kisiasa.
Mada mbalimbali zimekuwa zikijadiliwa ikiwemo zile zinazogusia utendaji wa rais Magufuli tangu alipoingia madarakani na mweleko wa baadaye wa taifa.
Baadhi ya wasomi wameonyesha kuridhishwa na utendaji wa rais Magufuli wakitolea mifano namna alivyodhibiti rushwa, kuleta nidhamu serikali na kupigania rasilimali za taifa. Wamebainisha baadhi ya mambo aliyoyazingatia tangu alipoingia madarakani wakisema kwamba yanaakisi misingi halisi ya kutaka kujenga taifa linalojitegemea.
Utendaji wa Rais Magufuli waangaziwa
Katika mchango wake mtoa mada kwenye mdahalo huo, Profesa Kitila Mkumbo ambaye yuko serikalini, alimtaja Rais Magufuli kama mwanasiasa aliyethubutu kufanya mambo mengi aliyoyaita magumu.
Kongamano linatoa fursa kwa washiriki kuchambua hali ya uchumi wa taifa na mwelekeo wa kisiasa Kongamano linatoa fursa kwa washiriki kuchambua hali ya uchumi wa taifa na mwelekeo wa kisiasa
Wasomi kwenye mdahalo huo unaohudhuriwa na wanazuoni mbalimbali, wamekuwa wakitofautiana kwa hoja na wakati mwingine wakiwafanya wafuatiliaji kaungua vicheko na kupiga makofi.
Msomi wa siku nyinyi wa masuala ya siasa na utawala, Profesa Rwekaza Mukandala amesema kipindi cha miaka mitatu ya Rais Magufuli kimejaribu kuchora dira lakini pia alibainisha changamoto zinazopaswa kutiliwa maanani ikiwamo vitendo vya rushwa na utendaji wa vyombo vya utoaji haki.
Uchumi umewafaidi wananchi moja kwa moja?
Kuhusu mwenendo wa uchumi ingawa baadhi yao wamesema umekuwa ukiendelea kukua katika kiwango cha kuridhisha hata hivyo baadhi walionyesha wasiwasi namna uchumi huo usivyogusa maisha ya watu moja kwa moja.
Mwanazuoni wa siku nyingi Profesa Issa Shivji amesema ni jambo la kufurahisha kwa taifa kuhimiza ujenzi wa viwanda lakini akaonya kuhusu njia zinazotumiwa kufikia ndoto hiyo.
Kongamano hilo linahudhuriwa kwa mara ya kwanza na Rais Magufuli aliyetajwa kama msikilizaji wa kawaida. Pembeni kwa kongamano hilo kumeshuhudiwa ulinzi mkali uliotanda eneo nzima la chuo kikuu hali ambayo baadhi ya wakosoaji wanasema haijapata kushuhudiwa hali kama hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

Mhariri: Iddi Ssessanga
DW SWAHILI 

Post a Comment

0 Comments