Urusi yateka meli za kivita za Ukraine - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, November 26, 2018

Urusi yateka meli za kivita za Ukraine

Urusi imezishambulia na kuziteka meli tatu za kivita za Ukraine zilizokuwa baharini katika rasi ya Crimea katika kisa ambacho kimezidisha uhasama baina ya mataifa hayo mawili.

Meli mbili ndogo za kivita, pamoja na meli moja ya kusindikiza meli ndizo zilizotekwa na wanajeshi wa Urusi. Wahudumu kadha wa meli za Ukraine wamejeruhiwa.

Leo Jumatatu, wabunge wa Ukraine wanatarajiwa kupiga kura kuidhinisha kuanza kutekelezwa kwa sheria za kijeshi.

Mzozo wa sasa ulianza pale Urusi ilipoituhumu Ukraine kwa kuingiza meli katika maeneo yake ya bahari kinyume cha sheria.

Urusi kisha iliweka meli kubwa ya kusafirisha mizigo na kuziba daraja la kuingia kwenye mlango wa bahari wa Kerch, njia pekee ya kuingia kwenye Bahari ya Azov na ambayo hutumiwa na mataifa yote mawili.
  
Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama na Ulinzi la Ukraine, Rais Petro Poroshenko alieleza vitendo vya Urusi kuwa "uchokozi usio na sababu na za kiwendawazimu."

Urusi imeomba kuandaliwe mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mkutano ambao balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema umepangiwa kufanyika saa tano asubuhi saa za New York (16:00 GMT) leo Jumatatu.

Uhasama umekuwa ukiongezeka katika Bahari Nyeusi na Bahari ya Azov katika rasi ya Crimea, eneo lililotekwa na Urusi mwaka 2014 kutoka kwa Ukraine.
  
Asubuhi, meli za kivita za Berdyansk na Nikopol, pamoja na meli ya kuzisindikiza Yana Kapa, zilijaribu kusafiri mji wa bandarini kwenye Bahari Nyeusi wa Odessa kuelekea Mariupol katika Bahari ya Azov.

Ukraine inasema Urusi ilijaribu kuzizuia meli hizo zisiendelee na safari yake, ambapo meli moja iliigonga meli ya Yana Kapa.

Meli hizo ziliendelea na safari kuelekea mlango wa bahari wa Kerch, lakini zikapata njia imezibwa na meli moja kubwa.

Urusi wakati huo ilikuwa imetuma ndege mbili za kivita na helikopta mbili ambazo zilikuwa zikipaa angani katika eneo hilo na kufuatilia mwenendo wa meli hizo.

Credit: BBC
Loading...

No comments: