Dereva Ahukumiwa Mwaka Mmoja Jela kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh 5,000 kwa Traffic


Dereva Ahukumiwa Mwaka Mmoja Jela kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh 5,000 kwa Traffic
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Luzango Khamsin amemhukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh 300,000 dereva wa gari aina ya Noah, Rashid Ally Katunda kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh 5,000 kwa askari wa usalama barabarani.

Kwa mujibu wa mashitaka, Dereva Rashid ambaye hufanya safari zake katika barabara kati ya Mikumi na Ifakara, alimpa rushwa askari Polisi E.6993 CPL. Elvis aliyekuwa akitekeleza majukumu yake katika barabara ya Ifakara – Morogoro ili asichukuliwe hatua za kisheria kwa makosa ya usalama barabarani ya kutokuwa na leseni ya udereva pamoja na uchakavu wa bodi ya gari yaliyokuwa yanamkabili.

Taarifa ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Janeth Machulya iliyothibitishwa na Msemaji wa Takukuru, Dorice Kapwani jana, Katunda alikamatwa na maofisa wa Takukuru Januari 29, 2018 na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ambapo alifunguliwa Kesi ya Jinai Namba 14/2018.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Ainainyi Minja aliielezea Mahakama kuwa Katunda anashtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 kama hati ya mashtaka ilivyofafanua.

Aidha, baada ya upande wa mashtaka kutoa ushahidi pasi na shaka, Mwendesha Mashtaka aliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na wengine wanaotenda makosa kama hayo.

Post a Comment

0 Comments