Asasi za Kiraia zaupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, zadai umelenga kuua Demokrasia nchini - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Friday, January 25, 2019

Asasi za Kiraia zaupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, zadai umelenga kuua Demokrasia nchini

Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza wakati wa Mkutano wa asasi za kiraia kujadili juu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo asasi sita zimeupinga muswada huo. Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe (wa pili kulia) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Fatma Karume wakizungumza na waandishi wa habari juu ya maoni ya asasi za kiraia juu ya Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa.


Taasisi sita za kiraia zikiongozwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zimetoa msimamo wao kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa unaotarajiwa kuwasilishwa Bungeni  huku wakisema endapo utapitishwa utaua demokrasia nchini.

Taasisi hizo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Twaweza,Baraza la Habari (MCT), Center for Strategic Litigation, pamoja na Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) ambazo kwa pamoja zimedai kuwa muswada huo si rafiki katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa nchini.

Akizungumza leo wakati wa Mkutano na waandishi wa habari, Rais wa TLS Fatma Karume amesema endapo muswada huo utapitishwa hakuna aatakayekuwa salama hata wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwanasheria huyo amesema muswada huo unakwenda kinyumne na matakwa ya Katiba inayotoa uhuru wa kijieleza na zaidi utaminya uhuru wa kushiriki kwenye shughuli za kisiasa ikiwamo zile za utoaji wa elimu ya uraia.

"Tangu lini tunaifanya elimu kosa la jinai? ina maana tunataka ni elimu gani mwananchi apate, hili ni jambo la kustaajabisha sana," alisema Karume.

Aliongeza, "Kitu nataka kuwaambia wana CCM wanadhani kwamba wapo protected (wanalindwa) hawapo protected kabisa kwasababu sheria ni msumeno inakata pamde zote,”.

Hatahivyo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole, kimeunga mkono muswada huo na kwamba utasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji kutokana na sheria iliyopo sasa kutoakisi mazingira ya sasa.

Polepole alisema si kweli kwamba sheria inampa madaraka makubwa Msajili wa Vyama huku akisema muswada utasaidia kujenga mfumo thabiti wa siasa ndani ya vyama.

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema muswada unampa mamlaka makubwa  Msajili waVyama ambaye amemfananisha kama refa wa mpira wa miguu ambaye ni shabiki wa timu inayoshindana.

"Refa ameajiriwa na timu moja inayoshiriki mashindano hivyo inakuwa ngumu kutenda haki katika kipindi chote cha mchezo,mshahara wake unalipwa na moja ya timu na timu hiyohiyo inaweza kumwondoa madarakani kama haijaridhishwa na utendaji wake" alisema.

Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema pamoja na kuwa muswada huo una mazuri machache ikiwamo kuongeza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za ruzuku, umegubikwa na mabaya ambayo yata athiri kwa kiasi kikubwa shughuli za siasa.

Massawe amesema endapo muswada utapitishwa, bado kuna nafasi ya kudai mabadiliko ya sheria au kupeleka pingamizi mahakamani.

Mapungufu yanayotajwa na asasi hizo ni pamoja na mamlaka makubwa ya Msajili wa vyama, kuminya uhuru wa kujieleza, adhabu kali kwa makosa ya kiutendaji, kutokuwapo kwa ujumuishwaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

 

Loading...

No comments: