Barabara ya Morogoro - Dodoma mawasiliano yarejea - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, January 17, 2019

Barabara ya Morogoro - Dodoma mawasiliano yarejeaNaibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, amewahakikishia wananchi na watumiaji wa  barabara ya Morogoro-Dodoma kuwa mawasiliano  ya barabara hiyo sehemu ya maingilio ya daraja la Dumila yamerudi kama ilivyokuwa awali.


Kauli hiyo ameitoa leo mkoani Morogoro, alipofika darajani hapo kujionea athari za mvua zilizosababisha kubomoka kwa daraja hilo na wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo kwa  takriban masaa saba.

“Kama mlivyoshuhudia tangu asubuhi tumeanza kazi za kurudisha mawasiliano katika barabara hii, matengenezo yakamilika na wananchi tayari wameshaanza kutumia barabara”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, ameupaongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkez na wadau wote waliojitokeza katika kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega ili kurudisha mawasiliano katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwa imara,  Serikali ipo katika mpango wa kuboresha barabara hiyo ambapo kwa sasa wataalam wanafanya usanifu wa barabara hiyo na pindi usanifu huo utakapokamilika basi ujenzi wake utaanza mara moja na wataanza na sehemu korofi.

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, amesema kuwa uongozi wa mkoa ulifika eneo la tukio na kuanza kushirikiana na TANROADS mkoa kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea mapema.
Loading...

No comments: