Lissu kuanza ziara Marekani, Ulaya - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, January 26, 2019

Lissu kuanza ziara Marekani, Ulaya


Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), kuanzia Jumatatu Januari 28, 2019 anaanza ziara katika nchi mbili barani Ulaya, baadaye atakwenda Marekani ambako pamoja na mambo mengine atatoa mhadhara wa kitaaluma na kufanya mahojiano na vyombo vya habari

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika nchi mbili barani Ulaya kuanzia Jumatatu Januari 28, 2019.
Katika nchi hizo mbali na kufanya vikao kadhaa na viongozi wa Serikali na jumuiya mbalimbali, pia atapata fursa ya kutoa mihadhara ya kitaaluma na kufanya mahojiano na vyombo vya habari.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Januari 26, 2019 na ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene inaeleza kuwa mbunge huyo wa Singida Mashariki atakuwa nchini Ujerumani kwa siku mbili, ambako atakutana na baadhi ya maofisa wa Serikali na wabunge wa Bunge la Ujerumani.
Baadaye Lissu ambaye bado yupo katika matibabu licha ya kuruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka 2017 akiwa Dodoma na watu wasiojulikana, atazuru makao makuu ya Jumuiya ya Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji.
Katika ziara yake hiyo ya Ubelgiji atakutana na baadhi ya watendaji wa jumuiya hiyo, wabunge wa EU na wanadiplomasia wa mataifa mbalimbali wanaowakilisha nchi zao EU.
Baada ya Ubelgiji, Lissu ataelekea Washington DC, Marekani kwa siku 10 ambapo mbali ya kukutana na Watanzania wanaoishi nchini humo, hasa katika maeneo ya Washington, Houston, Texas na Alabama, atakutana pia na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Wengine atakaokutana nao Marekani ni watendaji wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID) pamoja na kamati za mabunge yote mawili ya Marekani zinazohusika na uhusiano wa nje (Afrika).
Katika ziara hiyo, Lissu atapata fursa ya kuwasilisha mada juu ya masuala mbalimbali katika taasisi kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na Center for Strategic and International Studies (CSIS) na The Atlantic Council and the World Resources Institute (WRI).
Akiwa mjini Washington DC, Lissu atakutana na kufanya mahojiano na baadhi ya vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa.
Mnadhimu huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni atahitimisha ziara hiyo kwa kufanya mhadhara mkubwa wa umma katika Chuo Kikuu cha George Washington (GWU).
Chuo hicho ni moja ya taasisi kongwe na kubwa za elimu ya juu nchini humo na duniani kwa ujumla.
Loading...

No comments: