MTANZANIA PEKEE ALIYEFANYA MAAJABU FA ENGLAND - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Saturday, January 26, 2019

MTANZANIA PEKEE ALIYEFANYA MAAJABU FA ENGLAND


Michuano ya Kombe la FA nchini England inatarajiwa kuendelea leo Ijumaa na siku mbili za wikiendi hii, kuna vigogo wawili Arsenal na Manchester United watakuwa uwanjani.

Lakini wakati vigogo hao wakipambana, upande wa pili kuna Mtanzania ambaye anashika nafasi ya pili kwa ufungaji mabao katika michuano hiyo.

Inawezekana Watanzania wengi hawalijui hilo lakini ndiyo uhalisia wenyewe huo, Mtanzania huyo ni Adi Yussuf ambaye anaichezea timu ya Solihull Moors inayoshiriki Ligi Daraja la Tano England.

Yussuf siyo maarufu sana katika soka la Tanzania lakini amewahi kuitwa kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wakati huo akiwa anaichezea Mansfield Town iliyokuwa Ligi Daraja la Tatu.

Mshambuliaji huyo ambaye alizaliwa Tanzania kabla ya wazazi wake kuhamia England ambako ndiko alikokulia, amekuwa mshambuliaji tegemeo katika timu hiyo na licha ya kuwa timu yake imeshatolewa kwenye FA Cup, alifanikiwa kufunga mabao matatu na hivyo kuwa nyuma ya vinara kadhaa wanaoshika nafasi ya kwanza wakiwa na mabao manne kila mmoja.


Kijana huyo ambaye inaelezwa kuwa baba yake aliwahi kuichezea Coastal Union ya Tanga, hakupata nafasi nzuri ya kuichezea Taifa Stars kwa kuwa wakati alipoitwa mwaka 2016 aliandamwa na majeraha na hivyo kukosa nafasi nzuri ya kuliwakilisha taifa lake alikozaliwa.

FA CUP 2018/19
Msimu huu wa michuano hiyo timu yake ilianza raundi ya kwanza kwa kucheza dhidi ya Hitchin Townna wakashinda mabao 2-0, ilikuwa Novemba 11, 2018, alifunga bao moja kwa penalti katika dakika ya 72. Wakafanikiwa kusonga mbele.

Katika raundi ya pili ya kombe hilo, wakakutana na Blackpool, mchezo wa kwanza ukamalizika kwa matokeo ya 0-0, ilikuwa Novemba 30.

Desemba 18, timu hizo zikarudiana na ndipo wakatolewa kwa jumla ya mabao 3-2 katika dakika za nyongeza baada ya matokeo ya mabao 2-2 katika dakika 90, ambapo Yussuf alifunga mabao mawili katika dakika ya 33 na 51.

Wapinzani wao hao ambao wanacheza Ligi Daraja la Tatu wakiwa nyumbani walipata bao la ushindi katika dakika ya 105 kwa njia ya penalti.


ANAFANYA KWELI KWENYE LIGI
Katika ligi anayocheza inayojulikana kwa jina la National League ambayo kwa levo za ligi za England ni Ligi Daraja la Tano, Yussuf pia amekuwa na mchango mkubwa kwa kuwa hadi sasa timu yake inashika nafasi ya pili kati ya timu 24 zinazoshiriki:

Mbali na timu kushika nafasi ya pili, pia kwenye upande wa kufunga huku nako ameshacheka na nyavu mara 9, kinara akiwa na mabao 19.

ADI YUSSUF
Kuzaliwa: Februari 20, 1992
Umri: Miaka 26
Kuzaliwa: Zanzibar, Tanzania
Urefu: Futi 6 inchi 1
TIMU YA UTOTONI
2008–2011 Leicester City
TIMU YA WAKUBWA
2011 > Leicester City
2011 > Tamworth (mkopo)
2011–2013 > Burton Albion
2013–2014 > Lincoln City
2013 >Gainsborough Trinity (mkopo)
2014 >Harrogate Town (mkopo)
2014 >Histon (mkopo)
2014–2015 > Oxford City
2015–2016 >Mansfield Town
2016–2017 >Crawley Town (mkopo)
2017 > Grimsby Town
2017–2018 > Barrow 2
018– > sasa Solihull Moors
Maisha yake ya soka alianzia katika timu ya watoto ya Leicester City na baadaye akapandishwa timu ya wachezaji wa akiba lakini akashindwa kuonyesha kiwango na Mei 21, 2011 aliruhusiwa kuondoka akiwa mchezaji huru.

SOLIHULL MOORS F.C.
Ilianzishwa Julai 10, 2007, wakijulikana kwa jina la utani la The Moors, uwanja wao wa nyumbani ni Damson Park ambapo kocha wao wa sasa ni Tim Flowers.

RAFIKI YAKE MBWANA SAMATTA
Nje ya uwanja, Yussuf amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na Mtanzania mwingine anayefanya vizuri katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, Mbwana Samatta anayeichezea Genk. Wawili hao wamekuwa wakitumiana salamu kupitia mitandao yao ya kijamii hasa Twitter.

Samatta ameonekana mara kadhaa akimpongeza Yussuf kwa kufunga au kuonyesha uwezo wa juu katika mechi zake, naye Yussuf amekuwa akifanya hivyo pia kwa Samatta ambapo lugha kubwa inayotumika baina yao ni Kiswahili.

Msimamo Ligi Daraja la Tano
                                   P W D L Pts
  1. Leyton Orient 30 16 9 5 57
  2. Solihull Moors 30 17 6 7 57
  3. Salford City 30 16 8 6 56
  4. Fylde 30 14 11 5 53
  5. Wrexham 30 15 8 7 53
Wafungaji FA Cup
Madden Fleetwood 4
Toney Peterborough 4
May Doncaster 4
Jennings Tranmere 4
Yussuf Solihull Moors 3
Magennis Bolton 3

Wafungaji Nationa l League
Rowe D. AFC Fylde 19
Bonne M. Leyton 18
Rooney A. Salford 18
McCallum P. Eastleigh 15
Kedwell D. Ebbsfleet 12
Noble L. Hartlepool 12
Gaffney R. Salford 11
Muldoon J. Harrogate 11
Turgott B. Maidstone 11
Armstrong L. Gateshead 10
Boden S. Gateshead 10
Cheek M. Ebbsfleet 10
Clifton A. Maidenhead 10
Smith T. Barrow 10
Yussuf A. Solihull 9
Loading...

No comments: