RE: WAZIRI MAHIGA ASHIRIKI MKUTANO WA 38 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza kama kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye  Kikao Maalum cha 38 cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 30 Januari 2019 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 1 Februari 2019. Wengine katika picha ni Kapt. Mstaafu, Mhe. George Mkuchika (kushoto), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maejimenti ya Utumishi wa Umma na Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango. Anayeonekana nyuma ya Mhe. Mkuchika ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.
Mawaziri hao wakipitia nyaraka mbalimbali wakati wa kikao hicho
Mwenyekiti wa Kikao Maalum cha 38 cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Mhe. Kirunda Kivejinja (wa pili kulia), ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza hilo.
Ujumbe wa Burundi ukiwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Mawaziri
Ujumbe wa Kenya nao ukifuatilia kikao
Mjumbe kutoka Sudan Kusini (kushoto) akiwa katika meza moja na ujumbe wa Rwanda wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri


Ujumbe wa Uganda nao ukifuatilia kikao

Wajumbe wa Tanzania wakiongozwa na Mawaziri wakifuatilia kikao. Kulia ni Naibuu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi Amina KH. Shaaban
Dkt, Aloyce Nzuki, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa na Bw. Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Aziz Mlima (kushoto) kwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao cha Baraza la Mawaziri 
Wajumbe wengine wa Tanzania
====================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU MKUTANO MAALUM WA 38 WA  BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mkutano Maalum wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubabaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 1 Februari, 2019.

Mkutano huo ambao unaongozwa na Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Uganda ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Kirunda Kivejinja utajadili agenda mbalimbali muhimu ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda zingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa  kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2019.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 28 Januari kikifuatiwa na kikao cha Kamati ya Uratibu chini ya Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 29 Januri 2019.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo  unaongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuwahusisha pia Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa , Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Waziri Fedha na Mipango, Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Joseph Kakunda (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara na Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo.


Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Arusha.
30 Januari 2019
Post a Comment

0 Comments