SERIKALI KUTOTOA TENA LESENI MPYA ZA UWINDAJI, SABABU HII HAPA... - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, January 28, 2019

SERIKALI KUTOTOA TENA LESENI MPYA ZA UWINDAJI, SABABU HII HAPA...Wizara ya Maliasili na Utalii, haitatoa tena leseni mpya za uwindaji wa kitalii kwa kampuni ambazo zimeshindwa kulipa fedha za vijiji unapofanyika uwindaji.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alitoa kauli hiyo jana Jumapili Januari 27, 2019 wakati akizungumza na Mwananchi juu malalamiko ya vijiji 23 vya Longido mkoani Arusha vinavyoidai kampuni ya Green Miles Safaris Ltd kiasi cha Sh329 milioni.

Kampuni zaidi ya 47 zimepewa leseni za uwindaji wa kitalii katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na malipo mengine katika vijiji pia zinatakiwa kulipa kwa mwaka dola 5,000 kwa ajili ya mchango wa maeneo ya jamii.

Kanyasu amesema kuanzia sasa wizara hiyo, haitaipa leseni ya kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii ama utalii wa picha kampuni yoyote ambayo itakuwa inadaiwa hadi hapo itakapomaliza kulipa madeni.

Amesema licha ya kulipa kampuni hizo, zina jukumu la kuimarisha ulinzi katika maeneo yao, ili kupambana na vitendo vya ujangili na zikishindwa pia zinapoteza sifa ya kupewa kitalu.

Uongozi wa wilaya ya Longido pamoja na viongozi wa vijiji 23 mwishoni mwa wiki waliomba wizara ya maliasili na utalii, kuingilia kati mgogoro wa malipo dhidi ya kampuni hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema kampuni hiyo, imeshindwa kulipa fedha hizo za vijiji licha ya kuahidi kufanyika hivyo Januari 3 mwaka huu.

"Tulikaa nao kwenye vikao ili kutatua mgogoro, wakaahidi kulipa madeni ya vijiji lakini sasa wamepuuza na hata tukiwaita hawaji," amesema.

Mkuu huyo, pia ameeleza kusikitisha na kuuawa kwa twiga 16 katika kitalu cha kampuni hiyo ndani ya miezi mitatu mwaka jana, hali ambayo inaonyesha kuna udhaifu katika ulinzi.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Green Miles safari, Abdalah Salum Awadhi, amekuwa akipinga baadhi ya madeni katika vijiji na ameahidi akirejea nchini atatoa ufafanuzi.

Diwani wa kata ya Kitumbeine, Timotheo Laizer na diwani wa kata ya Mdarara, Alayce Moshau, waliomba wizara ya Maliasili na Utalii kuzitaka kampuni za uwindaji kuwa na mahusiano mazuri na jamii.

Kwa upande wake, katibu tawala wa wilaya hiyo, Toba Nguvila alisema kuanzia sasa vijiji vyote vyenye wawekezaji katika wilaya hiyo ni marufuku kuingia mikataba na wawekezaji bila mikataba hiyo kuridhiwa na bodi ya ushauri ya wilaya.

CHANZO: MWANANCHI
Loading...

No comments: