Serikali yatoa Vitambulisho vingine Milioni Moja, Watendaji waonywa dhidi ya udanganyifu. - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Monday, January 28, 2019

Serikali yatoa Vitambulisho vingine Milioni Moja, Watendaji waonywa dhidi ya udanganyifu.

Image result for Vitambulisho Magufuli

Rais wa Tanzania, Dkt John Magufuli akionesha mfano wa Kitambulisho cha Mjasiriamali Mdogo Desemba mwaka jana ambapo alitoa vitambulisho 670,000 ikiwa ni mpango wa Serikali kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwapunguzia kodi.Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amekabidhi vitambulisho 1.1 milioni vya  wafanyabiashara wadogo nchini ikiwa ni awamu ya pili ya ugawaji wa vitambulisho hivyo vilivyoanzishwa na Rais John Magufuli.

Hii ni awamu ya pili ya ugawaji wa vitambulisho  baada ya Desemba mwaka jana  Rais John Magufuli kutoa vitambulisho 670,000 kama sehemu ya kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwapunguzia mzigo wa kodi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Januari 28,2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema Balozi Kijazi amekabidhi vitambulisho hivyo kwa wakuu wa mikoa yote nchini Ikulu jijini Dar es salaam na kuwataka wakuu wa mikoa hiyo kuhakikisha vitambulisho hivyo vinatolewa kwa wahusika na kwa wakati.

Pia, Balozi Kijazi ameonya juu ya taarifa za kuwapo kwa baadhi ya watumishi wa halmashauri ambao wanaviuza vitambulisho hivyo kwa zaidi ya bei elekezi ya Sh20, 000 kwa kila kimoja.

“Wapo watendaji wetu ambao sio waadilifu wanaviuza vitambulisho hivi kwa bei ya zaidi ya Sh20, 000 sasa ni jukumu lenu Wakuu wa Mikoa kudhibiti hiyo hali, mnapobaini mtendaji wa aina hiyo chukueni hatua immediately (haraka),” amesema balozi huyo.

Tofauti na awamu ya kwanza, awamu hii imeshuhudia ugawaji usio na uwiano ambapo baadhi ya mikoa imepata idai kubwa huku mingine ikipata idadi ndogo.Sababu za tofauti hiyo hazijawekwa bayana.

Desemba mwaka jana, Rais John Magufuli alitoa vitambulisho maalum 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania kwaajili ya kuwagawia wajasiriamali katika mikoa yao wakiwemo wa machinga vitakavyouzwa kwa Sh20, 000 kwa kila kimoja.

Siku hiyo kila mkuu wa alipokea vitambulisho 25, 000 ili wakavigawe kwa wafanyabiashara wa maeneo yao na fedha watakazopewa wakazilipe TRA.

Alivitoa wakati wa mkutano kati ya Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) na viongozoi mbalimbali wa umma nchini na kueleza kuwa vitambulisho hivyo ni maalumu kuwatambulisha wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Sh4 milioni.

Mkoa wa Dar es Salaam umepata vitambulisho 150,000 ukifuatiwa na Arusha yenye vitambulisho 100,000,Mbeya umepata vitambulisho 80,000.Mwanza umepata 55,000,Dodoma 50,000, na Kilimanjaro, Lindi na Mara (vitambulisho 40,000).

Mingine ni Geita, Iringa,Kagera,Katavi, Kigoma, Manyara ambayo yote imepata vitambulisho 35,000.

Loading...

No comments: