Watuhumiwa Kesi ya mauaji ya Dk Mvungi waomba Kufutiwa Kesi au kurudishwa polisi,


Mshtakiwa wa kwanza na wa pili katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaachia huru au kuwarejesha kituo cha polisi.

Washtakiwa hao ,Msigwa Matonya (35) na Mianda  Mlewa (45) wameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando baada ya wakili wa Serikali,  Jenipher Masue kueleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Washtakiwa hao walinyoosha mkono na kueleza kuwa shauri hilo ni la muda mrefu tangu mwaka 2013 na lilienda Mahakama Kuu na kuanza kusikilizwa lakini baadaye lilifutwa na kufunguliwa upya Novemba 2018.

"Mheshimiwa hakimu sisi tumechoka tuna familia na watoto tuna miaka sita tuko ndani na shauri hili lilishaenda  Mahakama Kuu likafutwa na kufunguliwa tena tunaomba Mahakama ituachie au kuturejesha kituoni," walidai washtakiwa hao leo Alhamisi Januari 17, 2019.

Watuhumiwa hao sita waliachiwa na Mahakama Kuu Novemba 26 na kufunguliwa shtaka kama hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya kuelezwa hayo Hakimu Mmbando aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 29 mwaka huu itakapotajwa tena.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 6, 2018, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, 2013, walifanya kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere wilayani Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi ambaye aliuawa wakati akiwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Post a Comment

0 Comments