Hatima ya Rufaa ya Mbowe na Matiku kujulikana kesho Machi Mosi - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, February 28, 2019

Hatima ya Rufaa ya Mbowe na Matiku kujulikana kesho Machi Mosi


Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
MAHAKAMA ya Rufani kesho Machi Mosi, 2019 inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

Katika uamuzi huo, mahakama inatarajiwa ama kukubali Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuendelea kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mbowe na Matiko, kutokana na kufutiwa dhamana katika kesi ya uchochezi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu au kuitupilia mbali rufaa hiyo.

 Mapema Leo Februari 28.2019  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi  ya uchochezi  inayowakabili vigogo hao na  wenzao saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliitwa kwa ajili ya kutajwa na
 Wakili wa Serikali, Wankyo Simon akadai kuwa bado wanasubiri hatua za rufaa zilizopo Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Profesa Abdallah Safari alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi kuwa ni muhimu mahakama ikapewa taarifa ya maendeleo ya rufaa zote na kwamba wao wamepata taarifa kuwa kesho  Mahakama ya Rufaa itatoa uamuzi dhidi ya rufaa hiyo

Wakili Wankyo alipoulizwa  alidai kuwa yeye bado hajapata taarifa kuhusu uamuzi huo na kwamba hata kama isingekuwa hivyo bado wanaomba tarehe ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 14, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Uamuzi huo wa rufaa  utatolewa na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti wao, Jaji Stella Mgasha, Mwanaisha Kwariko na Gerald Ndika  kutoa uamuzi huo baada ya Februari 18, mwaka huu kusikiliza rufaa hiyo iliyokatwa na DPP kupinga Mahakama Kuu kusikiliza rufaa ya kupinga kufutiwa dhamana iliyokatwa na wakina Mbowe.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka jana maeneo ya Dar es Salaam.
Loading...

No comments: