SBL, Polisi Dar kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda kupitia soka

Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Abdi Issango akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya' Usinywe na Kuendesha' Chombo cha moto inayoendeshwa na Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries (SBL) jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa SBL, John Wanyancha.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries (SBL) John Wanyancha akielezea umuhimu wa Mashindano ya Kamanda Cup katika kueneza elimu ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam, Februari 7, 2019 – Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inalenga kutoa elimu juu ya usalama barabarani kwa waendesha wa bodaboda zaidi ya 1000, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na watumiaji wengine wa barabara jijini Dar es Salaam kupitia kampeni yake ya ‘Usinywe na Kuendesha (Don’t Drink and Drive).
Ili kufanikisha lengo hilo, SBL kwa kushirikiana na jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, itayatumia mashindano ya mpira wa miguu  yajulikanayo kama ‘Kamanda Cup’ kwa siku za mwisho wa juma yatakayofanyika katika viwanja mbalimbali vya michezo katika manispaa za Kinondoni, Temeke, Ilala, Ubungo na Kigamboni kueneza elimu ya matumizi sahihi ya pombe. Mashindano hayo ya yanayolenga kutoa elimu ya usalama barabarani yanashirikisha timu 120 za mpira wa miguu za waendesha bodaboda.
Akiongea hivi leo katika mkutano na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama barabarani, Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni ya SBL, John Wanyancha, amesema wachezaji watakaoshiriki katika mashindano hayo ya ‘Kamanda Cup’ wataelimishwa juu ya usalama barabarani pamoja na Unywaji wa Kistaarbu kabla ya kucheza mechi zao.
“Pia tutawapatia wachezaji nyenzo za kuwaelimisha kuhusu masuala ya kunywa pombe kwa ustaarabu kama vile vipeperushi na kuwahusisha katika majadiliano yatakayosaidia kuwapa  mtazamo sahihi kuhusu matumizi ya vilevi,” amesema Wanyancha.
 “Unywaji wa kistaarabu maana yake ni zaidi ya kujiwekea kikomo cha kiasi gani cha kilevi utumie, inamaanisha pia kutokukubali kulewa au kutokuruhusu kilevi/pombe itawale maisha au mahusiano yako,” Wanyancha ameongeza.
Wiki iliyopita SBL iliendesha kampeni kama hii kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoani Mwanza ambapo mamia ya waendesha bodaboda, wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu pamoja na madereva wa vyombo vya moto binafsi na vya umma walipewa elimu kuhusu usalama barabarani na unywaji wa kistaarabu. Katika mafunzo hayo, SBL iligawa vipeperushi, fulana, stika za usalama barabarani, makoti ya usalama barabarani na vitu vingine vilivyobeba ujumbe wa ‘Usinywe na Kuendesha.’
Akiongea kuhusu mashindano ya ‘Kamanda Cup’ yaliyoaandaliwa na Polisi mkoani Dar es Salaam katika jitihada za kuimarisha usalama barabarani, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Fortunatus Muslimu, ameelezea tukio hilo kuwa ni jukwaa la kujifunzia masuala mbalimbali ya usalama barabarani kwa wachezaji pamoja na mashabiki watakaokusanyika kuangalia mechi hizo.
Muslimu amesema wachezaji pamoja na mashabiki watapatiwa elimu juu ya vyanzo na namna ya kuepuka ajali za barabarani, tatizo ambalo amesema kwa kiasi kikubwa limekuwa likisababishwa na madereva kushindwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani. 
“Kama kila dereva angekuwa anafuata kwa kikamilifu sheria na kanuni za usalama barabarani, ajali nyingi zingeweza kuepukwa”, amesema Musilimu.
Aliwahakikishia wananchi kuwa jeshi la polisi limejipana vizuri katika kuendelea kuwaelimisha watumiaji wa barabara ili kuhakikisha vyanzo vya ajali barabarani kama vile kuendesha kwa mwendo wa kasi, madereva kuendesha wakiwa wamelewa kupakia mizigo kupita kiasi na vianzo vingine kama hivi vinatokomezwa.

Muslimu aliishukuru SBL na wadau wengine kwa kuunga mkono juhudi za jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kupitia kampeni ya Usinywe na Kuendeha, jambo ambalo amesema litatia chachu zoezi la utoaji elimu kwa madereva na umma kwa ujumla juu kuhusu masuala mbalimbali ya usalama barabarani.

Post a Comment

0 Comments