Maafisa Utamaduni Waagizwa Kusimamia na Kutekeleza Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 - MWANAHARAKATI MZALENDO ™

Breaking

Thursday, February 28, 2019

Maafisa Utamaduni Waagizwa Kusimamia na Kutekeleza Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997


 

Maafisa Utamaduni Waagizwa Kusimamia na Kutekeleza Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997.
 Na.Shamimu Nyaki -WHUSM 
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo,  Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe amewaagiza Maafisa Utamaduni wa Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia na kutekeleza Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kwakua ni ndio muongozo wa kukuza na kuendeleza Utamaduni wa Nchi yetu.

Mhe. Waziri ameyasema hayo leo Jijini Dodoma  alipokuwa akifungua  Kikao Kazi  cha 11 cha Maafisa Utamaduni wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kilichoandaliwa na Wizara yake ambapo amesema kuwa   Kikao kazi hicho kitasaidia kuibua changamoto na kutafuta namna ya kuzikabili pamoja na kubuni fursa zilizopo katika Sekta hiyo.

“Naamini kikao kazi hiki kitatoka na maadhimio mazuri yanayoelezea namna bora ya kuondoa mmomonyoko wa maadili unaotokana na kudharau, kupuuza na kudidimiza mila na desturi za nchi yetu na kufuata tamaduni za nje zisizofaa.”  Amesema Dkt Mwakyembe.

 Aidha Mhe. Mwakyembe  amewataka maafisa Utamaduni hao kutumia falsafa ya  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere inayosema, "Utamaduni ni kielelezo cha uhai na Utashi wa Taifa lolote lile, hivyo Taifa lisilo na Utamaduni ni Taifa mfu". Hivyo amewataka Maafisa hao kutumia taaluma yao kuwahimiza Watanzania kujivunia Utamaduni wetu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi. Susan Mlawi ameeleza kuwa kikao hicho kitakumbusha Maafisa Utamaduni kujadili mambo mbalimbali ya msingi, kubaini fursa pamoja na kuweka maazimio yatakayosaidia kuendeleza Utamaduni wa nchi yetu.

Kikao kazi hicho kinaongozwa na kauli mbiu isemayo “Umoja Upendo na Kazi Asili ya Utamaduni wetu”
Mbali na hayo Waziri, Dkt.Mwakyembe ametoa salamu za pole kwa Uongozi na Wafanyakazi wa Clouds Media Group, ndugu jamaa na marafiki kufuatia  kifo cha aliyekuwa Muanzilishi na Mkurugenzi wa Uzalishaji Vipindi Clouds Media Group Bw. Ruge Mutahaba ambaye alifariki jana Nchini Afrika Kusini. 

Katika hatua nyingine Mhe.Waziri Mwakyembe ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini  kumchukilia hatua za kinidhamu Msanii wa muziki wa kizazi kipya Godfrey Tumaini maarufu kama Dudu Baya kutokana na maneno aliyoyatoa ya kumdhihaki marehemu Ruge Mutahaba aliyekuwa Muanzilishi na Mkurugenzi wa Uzalishaji Vipindi Clouds Media Group ambaye alifariki jana Nchini Afrika Kusini.

Loading...

No comments: